30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Hatari watumiaji dawa za kulevya

  • Sasa wahamia matumizi ya ‘sumu ya panya’
  • Yaelezwa watumiaji uharibu figo, ini hadi kifo
  • Mamlaka ya Dawa za Kulevya yatoa neno

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

WATUMIAJI wa dawa za kulevya nchini, maarufu kama mateja, wameanza kugeukia dawa zenye uwezo wa kuua panya kutokana na kuadimika kwa dawa hizo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamishna wa Kinga na Tiba katika Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Dk. Peter Mfisi alisema tayari wameshabaini tatizo hilo na wanachukua hatua kuweza kuwanusuru watumiaji hao.

Dk. Mfisi alisema katika uchunguzi wao wamebaini kuwa watumiaji wengi wamekuwa wakitumia dawa zilizochanganywa na dawa za usingizi au za kutuliza maumivu zilizoko kwenye kundi la Indocid, ambazo ni hatari kwa afya zao.

Alisema kwa kawaida dawa hizo ambazo ni kwa ajili ya binadamu hutumiwa kwa maelekezo maalumu na daktari kwa wahitaji, lakini iwapo zitatumika kwa ajili ya kuulia panya pia huweza kuwaathiri na kusababisha kifo kwa viumbe hao.

“Dawa hizo huwa zinasababisha kukwangua utumbo na kusababisha damu kuvuja kwa ndani, kwa hiyo kama panya akila kidonge kimoja tu anaweza kufa, kwa sababu kutasababisha kuvuja damu na hata kuharibu utumbo wake. Baadhi ya watu hutumia vidonge hivyo kuwatega,” alisema.

Dk. Mfisi alisema kuwa wapo watu ambao hutumia dawa hizo kuua panya na zinaonesha mafanikio, kutokana na mfumo wa ulinzi wa viumbe hao kushindwa kuzihimili.

Alisema uchunguzi wao umebaini kuwa kutokana na kuzibwa kwa mianya mingi ya uingizaji dawa za kulevya nchini, kazi ambayo bado inaendelea, baadhi ya waingizaji wa dawa hizo waliofanikiwa kupenyeza wamekuwa wakitumia vidonge hivyo kuongeza uzito wa dawa zao ili kupata faida kubwa.

Dk. Mfisi alisema wengi wamekuwa wakiongeza dawa hizo kwenye heroin.

“Wanaweza kutafuta vidonge na kuongeza. Huchanganya kilo moja ya heroin na hadi kilo mbili za dawa hizo,” alisema.

Alisema kutokana na hilo, watumiaji wa heroin ambao nao huzipata kwa shida, hutafuta dawa hizo na kuziongeza katika unga huo bila kujua kuwa tayari umeshachanganywa, hivyo kujiongezea madhara maradufu na kwa kasi zaidi.

“Hizi Indocid ni miongoni mwa dawa za kutuliza maumivu. Wanapozichukua na kuchanganya kwenye heroin madhara yake yanakuwa makubwa zaidi na kuharibu figo na ini.

“Kwa kuwa wanatumia dawa hizo kinyume na utaratibu, wanavuruga upatikanaji wa dawa hizo ambazo huingizwa nchini kwa kazi maalumu na kusababisha uhaba usiotarajiwa,” alisema Dk. Mfisi.

Alisema wajibu wao kwa sasa ni kuhakikisha wanaendelea kuchunguza, kubaini na kuwakamata wote wanaojihusisha na uuzaji wa dawa hizo za hospitali kwa ajili ya matibabu nje ya utaratibu, na kuwanasa watumiaji wa dawa hizo.

Dk. Mfisi alisema kwa sasa wanaendelea kutoa elimu kwa watumiaji wanaozichanganya dawa hizo na dawa za kulevya kuhusu madhara yake.

Alisema tatizo hilo linaongeza madhara kwa kuwa hata heroin inayofanikiwa kupenya nchini siyo halisi bali ni ile chafu, ambayo upatikanaji wake ni wa bei nafuu kuliko dawa nyingine za kulenya, hivyo kuichanganya na dawa hizo ni hatari zaidi.

Kuadimika kwa mihadarati kama cocaine na heroine ni matokeo ya juhudi za Serikali kupambana na uingizwaji na usambazaji wa dawa hizo haramu nchini.

MTANZANIA lilimtafuta Dk, Mfisi baada ya taarifa ya BBC iliyoeleza kuhusu waraibu wa dawa za kulevya nchini kuchanganya sumu ya panya na dawa nyingine haramu za kulevya kama bangi na kisha kuvuta pamoja.

Kwa mujibu wa BBC, upatikanaji wa sumu ya panya ni rahisi sana hasa katika maduka ya bidhaa za nyumbani na kwenye masoko, na huuzwa kwa bei ya chini.

Si rahisi kumtilia shaka mnunuzi wa sumu ya panya, kufanya hivyo si kinyume cha sheria. Ila kwa sasa kinachosalia baada ya manunuzi ni jinsi gani sumu hiyo inaenda kutumika.

BBC ilieleza kuwa wakati mamlaka nchini zikiendelea kupiga hatua dhidi ya wafanyabiashara wakubwa na wa kati wa dawa za kulevya, ni dhahiri kuwa bado kuna changamoto kubwa ya kudhibiti watumiaji ambao kila uchao wanatafuta aina mpya ya dawa kukata kiu ya uraibu wao.

Mwaka jana ilielezwa kwamba waraibu wa mihadarati nchini wamegeukia dawa za usingizi kama njia mbadala baada ya kuadimika kwa dawa za kulevya.


- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles