29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Serengeti Boys hii na ile tunaendaje Brazil?

MOHAMED MHARIZO-DAR ES SALAAM

HISTORIA ya safari ya timu ya taifa ya vijana ya Tanzania walio chini ya miaka 27 ‘Serengeti Boys’ ilianzia mbali kwa juhudi kubwa ili nasi tuweze kusikia kwenye soka huko duniani.

Lakini hata hivyo kikosi hicho juzi kilishindwa kufuzu kusonga mbele, baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-2  kutoka kwa Angola.

Matokeo hayo yaliweza kuhitimisha safari ya kikosi hicho cha vijana katika  michuano hiyo ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) U-17.

Serengeti Boys iliandaliwa kwa vijana kusakwa na kuweka kambini enzi ya utawala wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Nakumbuka katika miaka ya 2015 programu nyingi za soka la vijana zilishamiri ikiwemo ya Alliance kule jijini Mwanza iliyokuwa na vijana wengi kuanzia miaka 13-17 walioweka tayari kwa mashindano ya Fainali za Afrika chini ya miaka 17 zilizofanyika nchini Gabon mwaka 2017.

Pamoja na kuandaliwa kwa vijana hao kwa muda mrefu, bado kulikuwapo na changamoto ya uzoefu katika kusaka tiketi ya kufuzu kwa michuano hiyo.

Tulicheza hatua ya mchujo ili tufuzu kwa mashindano hayo ya Gabon, lakini pamoja na maandalizi bado vijana wetu wakakumbana na changamoto ya wachezaji wenye umri mkubwa kutoka kwa timu walizokutana nazo na hasa Congo Brazzaville.

Katika kuwania kufuzu kwa fainalizi hizo za Gabon, Serengeti Boys ilifungwa lakini ikakata rufaa kwenye Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likitaka mchezaji Langa Bercy apimwe umri wake kwa kutumia kifaa cha MRI.

CAF chini ya Rais wake wa kipindi hicho, Issa Hayatou ikaagiza mchezaji huyo asafirishwe hadi mjini Cairo, Misri kwa ajili ya kufanyiwa vipimo hivyo, hata hivyo hakufikishwa na hivyo Congo Brazzaville ikaondolewa kwenye fainali hizo za Afrika zilizofanyika Gabon.

Serengeti Boys ikatusua na kushiriki kwa mafanikio fainali hizo ingawa haikupenya kwenye hatua ya nusu fainali kutokana na kushinda mchezo mmoja, sare moja na kufungwa mmoja.

Timu hiyo iliyokuwa chini ya Mdenmark Kim Poulsen, ilirejea nyumbani Tanzania kujipanga upya.

Lakini ikumbukwe kuwa mwaka 2015, CAF iliipa Tanzania uenyeji wa kuandaa mashindano hayo ya Afrika kwa vijana mwaka 2019.

Wakati timu hiyo ikiendelea TFF ikaachana na Kim Poulsen, ambaye mkataba wake unadaiwa ulisitishwa na timu hiyo kuachwa chini ya uongozi wa kocha mzawa Oscar Mirambo.

Watanzania wakawa na imani na Serengeti Boys iliyoachwa kwa Mirambo wakiamini kuwa viatu vya Poulsen vitamtosha kwa kuwa alikuwa msaidizi wake.

Timu hiyo licha ya kuwa ikisubiri mashindano hayo ya Afrika 2019 kwa kuwa wanafuzu moja kwa moja kama nchi jirani, ilipata maandalizi ya kutosha.

Serengeti Boys ikashiriki mashindano ya kufuzu Afcon U-17 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam mwaka 2019 chini ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Serengeti Boys pia ilishiriki mashindano ya maandalizi kule nchini Uturuki pamoja na mashindano yale yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka la Rwanda na vijana hao wa Mirambo walitwaa taji hilo.

Maandalizi ya Afcon U-17, 2019

Kama ilivyo desturi mara baada ya CAF kupitisha nchi mwenyeji, utaratibu unaofuata huwa ni ukaguzi wa miundombinu, hoteli pamoja na mambo mengine ili mashindano yachezwe vizuri.

Na kama kuna dosari, CAF hutoa maelekezo ya mambo gani yafanyike na wakaguzi hao kutoka kwenye shirikisho hilo hutoa ripoti na uenyeji wa nchi husika unaweza kutenguliwa, kwani hilo si jambo geni.

Zipo nchi zilipokwa uenyeji na CAF kutokana na kutokidhi vigezo.

Lakini kwa Tanzania hilo halikuwepo na maandalizi yalikuwa yakifanyika kwa kufuata maelekezo ya CAF kama walivyotaka.

Agosti, 2028 Rais wa sasa wa CAF Ahamd Ahmad, alisema  ameridhishwa na maandalizi ya mashindano ya Afrika ya vijana walio chini ya miaka 17.

Ahmad alisema hayo wakati alipozungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay, Dar es Salaam.

Rais huyo wa CAF pia alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba shirikisho hilo halitafanya mabadiliyo yoyote ya ratiba yatakayofanyika kuhusu wenyeji wa mashindano na kwamba CAF itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha mashindani hayo.

Rais huyo wa CAF alikuja nchini kwa ajili ya kuongoza mkutano maalum wa mabadiliko ya katiba ya Baraza la Vyama vya Soka katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), uliofanyika jijini Dar es Salaam nav kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi wanachama wote 12 wa CECAFA wakiwemo marais.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa alisema michezo yote itafanyika jijini Dar es Salaam.

Safari ya Serengeti Boys Total U-17 Afcon-2019

Hatimaye ukawadia muda wa kufanyika mashindano hayo ya mwaka huu ya Fainali za vijana Afrika (Total U-17 Africa Cup of Nations).

Mashindano hayo ya wiki mbili kuanzia Aprili 14 hadi 28 yanashirikisha nchi nane zilizogawanywa kwenye makundi mawili yaani A na B.

Wenyeji Tanzania (Serengeti Boys) wamepangwa kundi A wakiwa na Nigeria, Angola na Uganda.

Katika kundi B kuna Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.

Katika kuhakikisha kuwa vijana hao wa Serengeti Boys wanafanya vizuri na kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil baadae mwaka huu.

Serikali pamoja kutoa sapoti ya maandalizi kwa timu, lakini pia Rais Dk.John Magufuli kutangaza kutoa Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo hayo, bado ilitangaza mashabiki kuingia bure uwanjani.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza viingilio kuwa bure Aprili 14, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo  na kwamba Serikali imeamua kubeba gharama zote ili mashabiki waingie bure na kuishangilia Serengeti Boys ili itimize kufuzu Kombe la Dunia au kutwaa ubingwa huo.

Hata hivyo Serengeti Boys ilijikuta ikifungwa mabao 5-4 na Nigeria, katika mchezo huo wa ufunguzi mbele ya Waziri Mkuu na Rais wa CAF, Ahmad Ahmad na vingozi mbalimbali.

Timu hiyo ilijikuta ikifungwa tena mabao 3-0 na Uganda katika mchezo wa pili.

Tofauti ya Serengeti Boys ile na hii

Kiuhalisia kikosi cha timu kilichoshiriki mashindano ya Gabon mwaka 2017 na hiki kinachoshiriki mashindano haya kina tofauti kubwa.

Kikosi kile vijana wa Gabon walikuwa na ari na nguvu, walipambana na hata kufukia hatua ya kushinda mchezo mmoja, sare moja na kufungwa mmoja.

Hawa wa sasa hivi wanazidiwa nguvu, maumbo yao madogo na wanashindwa kuleta ushindani.

Wamepoteza michezo miwili ambayo wangeshinda wangekuwa wamejihakikishia kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.

Lakini yawezekana kuondoka kwa Poulsen ikawa sababu nyingine, kwa kuwa ni kocha mzoefu aliyekuwa na timu hiyo tangu wakati wa kusaka vipaji.

Serengeti Boys hii imekuwa dhaifu licha ya uwezo wa mchezaji mmoja mmoja kuonekana kama Kelvin John, Morice Abraham, Arafat Swakali, Agiri Ngoda na wengineo.

Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo, amekiri kuwa vijana wake ni wadogo ukilinganisha na wengineo wanaoshiriki mashindano hayo.

“Ukiangalia namna mashindano yalivyo vijana wangu wamejitahidi maana  ni wadogo, ukiangalia Cameroon unaona ni wakubwa lakini ndio wamefuzu vipimo vya MRI.

“Angalia Morocco au Guinea utaona hao ndio umri sshihi wa kucheza mashindano haya, mimi sio dokta lakini si muumini wa MRI,” alisema.

Alisema kuwa kutokuwepo kwa ligi za vijana pia ni tatizo kwa kuwa wachezaji wanakosa uzoefu na wao makocha wanakuwa na kazi kubwa ya kufundisha.

“Ukiangalia hawa wachezaji bado wadogo wanapaswa kuwa pamoja kwa muda mrefu, hakuna ligi na inapotokea kuna mashindano ndio unawakusanya,” alisema.

Mashindano hayo ya Afrika kwa vijana yatatoa timu nne, kila kundi timu mbili zitakazofuzu Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles