SEOUL, KOREA KUSINI
KIONGOZI wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, anatarajiwa kutembelea nchini Urusi mwezi huu ambako atakuwa na mazungumzo na Rais Vladimir Putin, huku hatua hiyo ikitajwa kuwa imewaudhi viongozi wa Serikali ya Marekani, ambao wako kwenye mnyukano mkubwa na Korea Kaskazini kutokana na mikutano yao kushindwa kupata suluhisho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Kremlin ya Urusi kwenda kwa vyombo vya habari juzi, mkutano kati ya Putin na Kim haujapangiwa tarehe rasmi, lakini unatarajiwa kuwakutanisha viongozi hao.
Mkutano huo umepangwa muda mfupi baada ya Korea Kaskazini kutoa mapendekezo kwa Serikali ya Marekani kumwondoa waziri wao wa mambo ya nje, Mike Pompeo kwenye Kamati ya majadiliano kati ya nchi hizo mbili.
Pia, Korea Kaskazini imeeleza kuwa imefanikiwa kufanya majaribio ya silaha mpya za kivita za kinyuklia. Hatua hiyo imetajwa kuwa pigo dhidi ya kiongozi wa Kamati ya Majadiliano ya Marekani, Pompeo.
Mkutano wa Kim na Putin utakuwa wa kwanza kuwakutanisha viongozi hao, ambapo utafanyika mjini Moscow nchini Urusi. Ikulu ya Kremlin imesema imemwalika Kim Jong Un kwenye mkutano huo, ambao utafanyika katika kipindi cha pili cha mwezi Aprili, lakini hakukuwa na taarifa nyingine zaidi.
Maofisa wawili wa Serikali ya Marekani, mshauri wa rais, Fiona Hill na Balozi maalumu Stephen Biegun nao walikuwa mjini Moscow kufanya mazungumzo na maofisa wa serikali ya Urusi.
Korea Kaskazini na Marekani zimekuwa na uhusiano wa mashaka wa kidiplomasia tangu kuvunjika kwa mkutano wa Kim na Trump mwanzoni mwa mwaka huu. Korea Kaskazini imemtaja Mike Pompeo kuwa kiongozi anayetakiwa kuondolewa kwenye wadhifa wake.