Maandamano katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum bado yanaendelea kurindima huku waandamanaji wakishinikiza jeshi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia
Waandamanaji hao wanasema kuwa hawataondoka barabarani hadi wapate mabadiliko ya kudumu.
Baraza la mpito linaloongozwa na jeshi limeahidi kuzingatia matakwa yao lakini waandamanaji wanahofia hatua waliopiga huenda ikahujumiwa ikiwa utawala utasalia mikononi mwa wanajeshi.
Wamejikusanya katika eneo kubwa la katikati ya mji wa Khartoum karibu na makao makuu ya kijeshi, hali ambayo imesababisha msongamano mkubwa.
Hatua hiyo imepelekea mashauriano ya ngazi ya juu huku wanasiasa na viongozi wa kijeshi wakilazimika kufanya kazi ya ziada kutafuta ufumbuzi wa suala hilo haraka iwezekanavyo.
Wachambuzi hata hivyo wanasema kujenga taifa litakalo heshimu utawala wa kidemokrasia baada ya kuwa chini ya utawala wa kijeshi kwa miaka 30 sio kitu ambacho kinaweza kufikiwa kwa muda wa wiki moja.