BARCELONA, HISPANIA
BAADA ya Barcelona kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Atletico Madrid juzi kwenye Uwanja wa Camp Nou, kocha wa timu hiyo, Ernesto Valverde, ameweka wazi kwa sasa hakuna wa kuwazuia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Kutokana na ushindi huo, Barcelona wanakuwa wanaongoza msimamo wa ligi huku wakiwa na pointi 73, baada ya kucheza jumla ya michezo 31, huku Atletico Madrid wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi 62, wakati huo Real Madrid wakiwa na pointi 60 katika nafasi ya tatu.
Mabao ya Luis Suarez na Lionel Messi ambayo yalifungwa katika dakika tano za mwisho kabla ya mchezo huo kumalizika, yaliweza kumfanya kocha wa Barcelona kuweza kuongea maneno ya kujiamini.
Hata hivyo, Barcelona walionekana kuwa na nguvu katika mchezo huo baada ya mshambuliaji wa Atletico Madrid, Diego Costa, kuoneshwa kadi nyekundu kutokana na utovu wa nidhamu katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.
“Hizi ni pointi tatu muhimu kwetu, tunakaribia kutwaa ubingwa, hivyo lazima tuendelee kushinda michezo yetu iliyobaki, lakini kazi kubwa naweza kusema tumemaliza dhidi ya Atletico Madrid.
“Tunayo furaha kubwa kwa kuwa wapinzani wetu Atletico Madrid wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi, hivyo ushindi huo unatufanya tuwe na amani kutokana na idadi ya pointi ambayo tumewaacha,” alisema kocha huyo.
Barcelona kwa sasa wanajiandaa na mchezo wao wa Jumatano dhidi ya Manchester United kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali ya kwanza, ambapo mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford kabla ya marudiano katika Uwanja wa Camp Nou.
Baada ya mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa, Barcelona watashuka tena dimbani kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya timu ambayo inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi, Huesca.