NEW YORK, MAREKANI
BODI ya Utendaji ya Benki ya Dunia imeridhia kwa kauli moja uteuzi wa David Malpass kuwa Rais wa 13 wa taasisi hiyo ya fedha kimataifa. Malpass, aliyekuwa ofisa mwandamizi kwenye Wizara ya Fedha nchini Marekani, ataanza kutumikia wadhifa huo keshokutwa na hivyo kuchukua nafasi ya Jim Yong, aliyejiuzulu miaka mitatu kabla ya kumalizika kwa muhula wake.
Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani, kuteuliwa kwa Malpass kumesababisha lawama duniani kote, kutokana na msimamo wake wa kuikosoa Benki ya Dunia mara kwa mara. Hata hivyo, alipokuwa kwenye Wizara ya Fedha alisaidia katika juhudi za kupatikana kiasi cha dola bilioni 13 kwa ajili ya kuongeza mfuko wa Benki hiyo.