Na CHRISTINA GAULUHANGADAR ES SALAAM
ILI kupunguza vifo vya akina mama na watoto elimu ya afya ya uzazi ni muhimu ndani ya jamii.
Miaka ya hivi karibuni, takwimu za afya zilikuwa zinaonyesha wanaongoza kwa vifo ni wanawake na watoto.
Vyanzo vya vifo vingi hapa nchini vilikuwa vikitokea wakati wa kujifungua au kukosa huduma za afya na vingine ni uzembe wa wahuhumu wa afya.
Wapo wazazi ambao wamekuwa wakisahau kabisa majukumu yao kwa kushindwa kutoa elimu ya afya kwa watoto wao.
Hali hiyo imekuwa ikichangia watoto wengi kujikuta wakipata ujauzito wakiwa na umri mdogo jambo ambalo linachangia kufariki wakati wa kujifungua.
Pia ukosefu wa elimu umekuwa ukisababisha watoto wengi kupata magonjwa ya kuambukiza.
Wazazi inatakiwa tujenge urafiki na watoto wetu tusiwe maadui, kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kufahamu hata mabadiliko yake ya mwili.
Mzazi ukiwa adui kwa mwanao, hawezi kukushirikisha kwa lolote na kumuweka zaidi mtoto wako kwenye hatari ya kuingia kwenye makundi yasiyofaa, mwishowe kupata magonjwa ya kuambukiza.
Ifike wakati mzazi au mlezi kila mmoja akatambua nafasi yake kuanzia ngazi ya familia ili kujenga taifa lenye afya na amani ya kweli.
Ni wazi kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kuwa mlezi wa watoto wote kwani hata mtoto wa jirani ni wako, kamwe usisite kumuonya pindi unapoona amekosea.
Ipo haja kwa kuwajengea hata uwezo wa elimu ya afya watoto kwa kuwatafutia wataalam wa afya na kuwapa mafunzo ambayo yanatolewa kwa bei nafuu.
Mafunzo hayo kama kuna ushirikiano mzuri hata na uongozi wa mitaa na vijiji yanaweza kupatikana bure kupitia kwa maofisa maendeleo.
Ni imani yangu, wapo wataalam ambao wanafahamu afya ya uzazi na hata ya mazingira ambao wanaweza kupatikana bila gharama yoyote, kwani elimu watakayoitoa itasaidia kutokomeza magonjwa na hata utunzaji mazingira.
Ninasema hivyo kwakuwa afya ndio kila kitu, pindi inapotokea mtu kuumwa hata utendaji kazi unapungua.
Hivyo wazazi tushirikiane kujenga taifa lenye afya na malezi bora.