MOSCOW, URUSI
WAZIRI Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajia kukutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini hapa kesho.
Taarifa ya Ofisi ya Kiongozi huyo iliyotolewa jana haikufafanua zaidi kuhusu undani wa ziara hiyo, lakini inafanyika ikiwa ni siku tano kabla ya uchaguzi mkuu wa Aprili 9, ambao utakuwa na mchuano mkali.
Juzi Netanyahu aliwaambia waandishi wa habari kuwa yeye na Putin walizungumza kwa njia ya simu juu ya masuala ya Syria, ambako vikosi vya Serikali ya Rais Bashar al-Assad vinavyoungwa mkono na Urusi vimekuwa vikipata ushindi dhidi ya waasi, baada ya miaka minane ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Wiki iliyopita, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuitambua Milima ya Golan iliyoko Syria kuwa ni sehemu ya ardhi ya Israel, hatua ambayo imezua ukosoaji mkali kutoka jumuiya ya kimataifa.