27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Filikunjombe Alivyokatishwa uhai

MTZ jmosi new july.indd*Shuhuda aeleza jinsi alivyoona helikopta ikiwaka angani kabla ya kuanguka
*Maiti zaharibika zashindwa kutambuliwa, ipo ya baba wa Jerry Silaa, Kapteni Silaa
*Yaelezwa helikopta hiyo iliwahi kumbeba Lowassa, Mbowe, Nassari alianguka nayo

Na Waandishi Wetu

ALIYEKUWA mgombea ubunge katika Jimbo la Ludewa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deo Filikunjombe, ni miongoni mwa watu wanne waliothibitika kufariki katika ajali ya helikopta iliyoanguka juzi usiku katika Pori la akiba la Selous.

Wengine waliofariki katika helikopta hiyo yenye namba 5Y-DKK ni pamoja na rubani, Kapteni William Silaa, ambaye ni baba wa mgombea ubunge wa Ukonga kupitia CCM, Jerry Silaa na abiria wengine wawili.

Akithibitisha taarifa hizo kwa vyombo vya habari jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Polisi, Paul Chagonja, alisema rubani, Kapteni Silaa aligundua hitilafu ya ndege hiyo mapema na alitoa taarifa kwa uongozi wa pori la Selous, lakini kabla hajapata msaada mawasiliano yalikatika na helikopta ikaanguka.

“Rubani wa helikopta hiyo alitoa taarifa mapema ya kuomba kutua kwenye uwanja wa ndege uliomo ndani ya pori hilo, lakini ghafla mawasiliano yalikatika. Waokoaji wamefika kwenye eneo la tukio na wamekuta miili ya marehemu ikiwa imeungua vibaya kiasi cha kutotambulika,” alisema Kamishna Chagonja.

Msaidizi wa Filikunjombe, Mathias Luoga, alisema helikopta hiyo iliyokuwa na abiria watatu na rubani ilikuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Njombe, lakini wakiwa angani katika eneo la Kilombero ikapata hitilafu na kuanguka katika Mbuga ya Selous.

Gazeti la MTANZANIA la jana liliripoti taarifa za awali likimnukuu Meneja wa Selous, Benson Kibonde, ambaye alisema  helikopta hiyo ilianguka karibu na Mto Ruaha, katika Kitalu cha Uwindaji cha R3.

Alisema taarifa za ajali hiyo walizipata kwa njia ya satellite kutoka kwa mwindaji mmoja ambaye akiwa katika hema lake ndani ya Pori la Selous katika Kitalu cha R2, alisikia kishindo cha helikopta ikianguka na kuona moshi upande wa Kitalu cha R3.

Alisema baada ya ajali hiyo kutokea, mwindaji huyo pia alitoa taarifa kwa Kampuni ya Uwindaji ya Foa Adventure ambayo imempeleka katika pori hilo.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, kutokana na eneo hilo kuwa karibu na Mto Ruaha, ilikuwa vigumu kwao kwenda kwa kuwa usiku ulikuwa umekwishaingia.

Jerry Silaa ndiye aliyekuwa mtu wa mwanzoni kabisa kuthibitisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa Instagram.

“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya uokoaji, imefanikiwa kufika kwenye eneo la ajali na kukuta abiria na rubani wote wamepoteza maisha.

“Nimepoteza baba na rubani mzuri wa nchi yetu, Capt. William Silaa, nimepoteza rafiki na kiongozi wangu, Mhe. Deo Filikunjombe. Nawapa pole wote waliopoteza ndugu zao. Nawaombea marehemu mapumziko ya amani. Nawashukuru wote walioshirikiana na familia katika uokozi.”

Aliwashukuru Rais Jakaya Kikwete, mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, IGP Ernest Mangu, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru, Kampuni ya Everest Aviation, wabunge, wakuu wa wilaya na maofisa wa TCAA.

TAARIFA YA TCAA

Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), ilitoa taarifa ya kuthibitisha ajali ya chopa hiyo aina ya AS-35.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chopa iliyopata ajali ilikuwa na namba ya usajili 5Y-DKK, mali ya Kampuni ya General Aviation Service ya jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa ndani ya chopa hiyo kulikuwa na abiria watatu pamoja na rubani wake ambao wote wamepoteza maisha.

Abiria hao ni pamoja na rubani, Kapteni William Silaa, Deo Filikunjombe, Kasambala Haule na Ediga Mkwela.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa helikopta hiyo iliondoka katika  Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) juzi saa 9:57 jioni na ilitarajiwa kufika Njombe saa 12:20 jioni.

TCAA ikinukuu taarifa ya  Kituo Kikuu cha kuongozea ndega cha Uwanja wa JNIA, yaani Area Control Centre (ACC), inaelezwa kuwa kilipokea taarifa za awali za ajali hiyo saa 11:54 kutoka kwa mmoja wa watumishi wa Flight  Link, aliyepigiwa simu na shuhuda wa ajali hiyo aliyekuwa kwenye vitalu vya uwindaji wa kitalii huko Selous.

Katika taarifa hiyo, shuhuda wa ajali hiyo alieleza kwamba chopa hiyo ilionekana ikiwaka moto wakati ikielekea kuanguka.

TCAA imesema kuwa timu ya utafiti na uokoaji wa mamlaka hayo kwa kushirikiana na Kampuni ya Ndege ya Everet ya Dar es Salaam ilikutana kwa haraka na  kujipanga kwa ajili ya zoezi la utafutaji na uokoaji juzi  usiku.

Hata hivyo, TCAA ilisema kuwa chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika na kwamba wataalamu wa uchunguzi wa ajali za ndege wanaendelea na uchunguzi.

HELIKOPTA ILIWAHI KUTUMIWA NA LOWASSA, MBOWE

Taarifa zilizokusanywa na gazeti hili, zinaeleza kuwa kabla ya ajali hiyo, helikopta hiyo iliwahi kutumiwa na wanasiasa maarufu nchini, akiwemo mgombea urais wa Chadema anayewakilisha Ukawa, Edward Lowassa, alipokuwa akitafuta wadhamini wakati akiwania urais kupitia  CCM Juni, mwaka huu.

Pia inaelezwa kuwa helikopta hiyo iliwahi kutumiwa na Chadema katika operesheni zake, ikiwemo ‘Operation Delete CCM’ na nyinginezo.

Zipo pia taarifa zinazoeleza kuwa iliwahi kutumiwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Geita, Joseph Kisheku, maarufu kama Msukuma.

MBOWE AELEZA ALIVYOWAHI KUITUMIA

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema chama hicho na kambi ya Ukawa imepokea kwa masikitiko taarifa za ajali hiyo, huku akieleza zaidi jinsi alivyomfahamu Kapteni Silaa.

“Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo. Kwa kuwa taarifa zimetolewa na Jerry Silaa, ambaye ni mtoto wa Kapteni Silaa, basi tunaziamini na tumepokea kwa mshtuko mkubwa,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Kapteni Silaa naye ninamfahamu… kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa sekta ya usafiri wa anga. Alikuwa rubani mzoefu kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati. Amesharusha ndege nchi za Kenya, Uganda hadi Congo. Amesharuka na ndege kwa zaidi ya saa 7,800,” alisema Mbowe.

Alisema licha ya ajali hiyo, Kapteni Silaa pia alipata ajali akiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari Julai 7.

“Tumefanya naye kazi sana kwenye operesheni zetu na amekuwa akifanya kazi bila kinyongo chochote. Kama unakumbuka kuna ajali ya helikopta aliyopata Mbunge Nassari, Kapteni Silaa ndiye alikuwa rubani na alifanikiwa kuepusha madhara. Isitoshe yule ni kaka yangu wa nyumbani, tunatoka wote Jimbo la Hai na tunashirikiana kwa mambo mengi,” alisema Mbowe.

Kuhusu Filikunjombe, Mbowe alisema alikuwa ni rafiki mkubwa wa kambi ya upinzani, licha ya kuwa chama tawala.

MIILI YAPELEKWA LUGALO DAR

Spika wa Bunge, Anne Makinda, ndiye aliyeongoza mapokezi ya miili ya marehemu hao jana katika lango namba 11 la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) jijini Dar es Salaam.

Msafara wa Spika Makinda uliwasili uwanjani hapo saa 11:25 jioni na kupokelewa na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah.

Muda mfupi baada ya msafara wa Makinda kuwasili, ndege iliyobeba miili iliwasili na msafara wa kuelekea Hospitali ya Jeshi ya Lugalo saa 12 jioni.

Awali msafara wa magari ulianza kuingia uwanjani hapo saa 10:00 jioni, kukiwa na magari manne ya kubebea maiti pamoja na magari mawili ya kubebea wagonjwa.

 

Magari hayo, mojawapo lilikuwa la Ofisi ya Bunge lenye namba STL 1307 pamoja na gari moja la wagonjwa la Manispaa ya Ilala linalomilikiwa na Hospitali ya Mnazi Mmoja yenye namba DFP 7119.

 

Msafara huo ulielekea moja kwa moja katika Hospitali ya Jeshi la Lugalo ambako uliwasili  saa 12:30 jioni, ambapo miili hiyo  ikiwa imefunikwa kwa plastiki  maalumu nyeusi ilibebwa kwenye machela.

MTANZANIA Jumamosi ambalo lilikuwa likifuatilia tukio hilo tangu uwanja wa ndege, lilishuhudia miili hiyo ikitolewa katika gari la wagonjwa la Bunge, wakati mingine ilitolewa katika magari tofauti ambayo ni maalumu kwa ajili ya kubebea maiti na kisha kuingizwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya chumba hicho, Mgombea ubunge wa Jimbo Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo ambaye ni Msimamizi wa shughuli za msiba wa Filikunjombe, Zitto Kabwe, alisema kuwa wamepokea miili na kuiingiza ndani na zoezi lililokuwa likiendelea ni la utambuzi wa miili hiyo.

“Siwezi kuongea kama rafiki wala mfanyakazi mwenzangu, sitaweza kueleza kabisa, kikubwa ni kuwa miili imeharibika na sasa tunaendelea na zoezi la utambuzi, maana watu wameungua na wapo wanne, hatuwezi kujua nani ni nani, hivyo wataalamu wanaifanyia utambuzi kwa kushirikiana na ndugu,” alisema Zitto.

Alisema baada ya utambuzi taratibu za maizishi zitaendelea na kwamba maziko yatafanyika haraka kwakuwa maiti zimeharibika.

MAMBO MUHIMU YA KUKUMBUKWA FILIKUNJOMBE

Marehemu Deo Filikunjombe alikuwa miongoni mwa wabunge vijana wenye misimamo thabiti isiyoyumbishwa.

Aina ya siasa aliyoiendesha ilivutia wengi, pamoja na kuwa mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini kwa msimamo wake alidiriki hata kukikosoa chama chake hadharani na hakusita kuweka wazi msimamo wake kwa kuangalia masilahi ya nchi.

Umahiri wake wa kusimamia ukweli ulimpa fursa kubwa ndani ya Kamati ya PAC, ambayo aliiongoza kama Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Marehemu Deo Filikunjombe amefanya mambo mengi na yenye historia ya aina yake.

Sakata la Escrow

Aliitumia  vizuri nafasi yake PAC kuandaa na kuiwasilisha ripoti nzima ya sakata la ukwapuaji wa Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT).

Ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa mwishoni mwa mwaka jana, iliitikisa nchi kwa kufichua miamala iliyotumiwa kuchota fedha hizo, pia iliainisha majina ya wahusika.

Madudu ndani ya mashirika ya umma

Kutokana na uwezo mkubwa wa kusimamia ukweli pasipo kutetereka, marehemu Filikunjombe kwa kushirikiana na timu nzima ya kamati ya PAC kwa pamoja waliweza kubaini ufisadi katika mashirika mbalimbali ya serikali, kama vile madudu yaliyobainika ndani ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Benki ya NBC.

Maendeleo Jimbo la Ludewa

Katika kipindi cha miaka mitano ya ubunge wa Jimbo la Ludewa, Marehemu Filikunjombe alifanikiwa kuchochea maendeleo ya jamii katika jimbo lake. Kwa picha iliyokuwa wazi marehemu alitazamiwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Msimamo wake dhidi ya Waziri Mkuu

Wakati wa sakata la kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kumng’oa madarakani Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Marehemu Filikunjombe hakuonyesha woga, alisimama mbele na kumnyooshea kidole Waziri Mkuu na kumwambia bayana kuwa anatetereka kuliongoza Baraza la Mawaziri.

Katika moja ya michango yake kwa mijadala ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Filikunjombe aliitaka Serikali kuchukua hoja za wapinzani na kuzifanyia kazi, jambo lililomkera Pinda.

Mawaziri wachapwe viboko

Filikunjombe pia aliwa kuliomba Bunge kubadilisha kanuni ili aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Chakula, Mhandisi Christopher Chiza, achapwe viboko bungeni.

Huku akiomba mwongozo kwa Spika Anne Makinda, Filikunjombe alisema kanuni hiyo iruhusu mawaziri wote wanaoshindwa kujibu maswali ya wabunge kwa ufasaha, wachapwe viboko na kutolea mfano wa Waziri Chiza kwamba, alipaswa kuchapwa viboko kwa kushindwa kujibu swali la Mbunge wa Mwibara, Kange Ligola (CCM).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles