24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

JK aitaka Taasisi ya Sayansi za Bahari kuwekeza katika utafiti

NA OSCAR ASSENGA, PANGANI

RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete, ameitaka Taasisi ya Sayansi za Bahari iliyopo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwekeza zaidi katika utafiti, ili waweze kupata maendeleo makubwa.

Kikwete, ambaye ni Mkuu wa UDSM, alitoa kauli hiyo mjini hapa juzi, alipofanya ziara ya kutembelea taasisi hiyo iliyopo Pangani.

Alisema uwekezaji katika utafiti ndicho kichocheo kikubwa kinachoweza kuwapa mafanikio na kuwataka kuweka msukumo katika suala hilo.

“Nimefurahi kwamba taasisi hii ipo kwa ajili ya bahari eneo la viumbe vya majini, hakuna taasisi nyingine kubwa kushinda nyie, mkibaki kuangalia viumbe vya baharini majini na kusahau na vilivyopo maji baridi kutakuwa na ombwe, lakini nafurahi hapa mmeanza kufanya utafiti wa viumbe wa maji baridi,” alisema.

Kikwete alisema taasisi hiyo imeanzishwa kwa ajili ya taaluma kubwa ya viumbe vya bahari, huku akiwataka waitumie kuingiza katika viumbe wa maji baridi.

Pia alisema ili kuibua mambo makubwa ya maana ya majini, lazima wahakikishe wanawekeza katika utafiti ambao ndio unaweza kuwafikisha katika mafanikio.

“Mkitaka kupata maendeleo makubwa lazima muwekeza kwenye utafiti, wakati nilipokuwa Rais niliwahi kwenda Korea nikatembelea Kampuni ya Samsung na wale wakatupeleka sehemu yao wanayofanyia utafiti, wana wafanyakazi zaidi ya 10,000, wakilala wakiamka wana kompyuta mpya na kuwa na vitu vipya walivyovumbua, hivyo lazima tubadilike tufikie huko,” alisema Kikwete.

Alisema ndiyo maana Korea ya Kusini wamepiga hatua kubwa kwa sababu wamewekeza katika utafiti.

“Nimelifafanua hili kutokana na maombi yenu mliyonipa hapa nimeyapokea nayafanyia kazi, lakini lazima mtambue kwamba taasisi hiyo shabaha yake kubwa ni kufanya utafiti,” alisema.

Pia alisema dhumuni la ziara hiyo baada ya kupewa dhamana ya kuwa Mkuu wa UDSM na Rais Dk. John Magufuli ni kufahamu eneo lake la kazi.

Alisema chuo hicho kinafanya kazi kubwa tatu ambazo ni kufundisha, kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali na kufanya utafiti, ikiwamo kuhudumia jamii.

Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari, Dk. Magreth Kyewalyanga, alisema malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kutoa mafunzo ya uvunaji endelevu na uzalishaji wa mazao ya samaki baharini.

Katika utafiti wa uzalishaji wa mazao ya bahari, taasisi hiyo ilianza na kilimo cha mwani na uzalishaji katika miaka ya 1980 pamoja na utafiti wa ufugaji wa samaki aina ya mwatiko, ikiwamo uzalishaji wa lulu katika miaka ya 2000 na hatimaye utafiti wa perege kuanzia mwaka 2009.

Alisema mazao mengine yanayofanyiwa utafiti na majaribio ni pamoja na majongoo bahari, kaa koko, chaza na spirulina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles