DAMASCUS, SYRIA
VIKOSI vya Kikurdi vinavyopigania demokrasia nchini Syria (SDF) vimelisambaratisha kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS), kutoka kwenye ngome yao ya mwisho kwenye kijiji cha Baghouz kilichoko mashariki mwa Syria.
Tangazo hilo la SDF inayoungwa mkono na Marekani, linahitimisha uwepo wa wapiganaji wa IS ambao walijitangazia utawala wa khalifa mwaka 2014.
Msemaji wa SDF, Mustafa Bali, alitangaza ushindi huo kupitia ukurasa wake wa Twitter, akisema Baghouz imekombolewa.
“’Ushindi wa jeshi dhidi ya wapiganaji wa IS umekamilika,” alisema Bali.
Mkuu wa Uhusiano wa Mambo ya Nje wa SDF, Abdel Kareem Umer amesema hilo ni tukio la kihistoria, lakini ameonya kuwa ushindi huo haumaniishi ndiyo mwisho wa ugaidi au IS.
”Tumelisambaratisha jeshi la IS, tumeumaliza utawala wao. Lakini bado IS ina mizizi na itikadi zao zinaendelea katika maeneo, ambayo waliwahi kutawala kwa miaka kadhaa,” alifafanua Umer.
IS iliwahi kuyadhibiti maeneo makubwa ya Irak na Syria, ingawa katika harakati za kuyakomboa maeneo hayo, zilizoendeshwa na Marekani na washirika wake kwa muda wa miaka mitano, magaidi wengi na raia waliuawa.