27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Michepuko chanzo kuzaliwa watoto wengi wa kike

BENJAMIN MASESE- MWANZA

OFISA Programu ya Uzazi Salama kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Martha Shakinyau, amesema moja ya sababu za kuzaliwa kwa watoto wa kike wengi ni wanaume kuwa na ‘michepuko’ mingi jambo linalofanya wapoteze nguvu nyingi huko na kurudi nyumbani wakiwa wamechoka.

Shakinyau aliyasema hayo jijini hapa katika semina kwa waandishi wa habari na Jukwaa la Tanzania la Mawasiliano ya Afya kwa watu wazima linalolenga kuleta mabadiliko chanya ya tabia kwa jamii.

Alisema wanaume wengi wamekuwa wakilalamikia wake zao kujifungua watoto wengi wa kike kuliko wa kiume, wakati wao ndio wanasababisha hali hiyo kutokea.

“Ni kweli watoto wa kike katika ndoa wanazaliwa wengi kuliko wa kike, hata takwimu zilizopo zinaonyesha hivyo hivyo, sasa kwa maelezo ya awali nasema wanapaswa kutulia kwenye ndoa zao.

“Ukiwa na michepuko huwezi kupata mtoto wa kiume ndani ya ndoa maana utarudi nyumbani ukiwa na uchovu wakati nguvu kubwa umeiacha nje ya ndoa na ndio unapata mtoto jinsia ya kike.

“Pili wanapaswa kutambua unapokuwa na uchovu kisha ukafanya tendo lile, mbegu za kike zinakuwa na mbio kuliko za kiume, hivyo nawashauri wanaume waende vituoni ili wapate elimu na watajua lini na wakati gani wa kupata mtoto wa kiume.

“Pia tambueni kuwa mimba nyingi zinazotoka ni za watoto wa kiume, ujauzito wa mtoto wa kiume hauna uvumilivu pale mimba inapopata misukosuko,” alisema Shakinyau.

Aliwataka wananchi kuhudhuria kwenye vituo vya afya ili kupewa elimu ya namna ya kupata watoto wa kiume, huku akiwaonya mama wenye ujauzito wa wiki moja hadi 12 kutotumia dawa bila maelekezo ya wataalamu   kuepuka kujifungua mtoto mwenye ulemavu.

“Jambo la tatu ni kuwaonya wanawake ambao wana ujauzito wa kuanzia siku moja hadi wiki ya 12, wasitumie dawa za kienyeji ama za kitalaamu bila maelekezo ya daktari.

“Kipindi hicho ni cha uumbaji wa kiumbe kilicho tumboni, sasa ukimeza dawa ovyo zinakwenda kuharibu kiumbe kile na matokeo yake ni kujifungua mtoto mwenye ulemavu,” alisema.

Hata hivyo aliwataka mabinti nchini kutambua umri mzuri wa kuanza kupata mtoto ni kati ya miaka 20 hadi 35, huku akidokeza kwamba hata tendo la ndoa huwa zuri kuliko kuwahi kujifungua wakati viungo havijajiandaa.

Shakinyau alisema takwimu zinaonesha kwa mwaka mmoja wanawake milioni 2.8 hujifungua, kati yao 800,000 hupata matatizo mbalimbali ya ujauzito.

Alisema wanaopata matatizo wengi wao ni kundi la vijana wenye umri chini ya miaka 24, huku asilimia 34 tu ndio wanaofika katika vituo vya afya kujifungua.

Aliongeza kuwa wanawake 556 kati ya 100,000 wanafariki kutokana na ujauzito, hivyo Serikali imeamua kuungana na majukwaa mbalimbali ya wadau wa afya yakiwamo ya Naweza na Sitetereki yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) ili kutoa elimu kwa jamii juu ya kujikinga na malaria, maambukizi ya Ukimwi, kifua kikuu, vifo vya mama na mtoto.

Semina hiyo ya siku tatu imehudhuriwa na waganga wakuu wa mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Kagera, mwakilishi wa USAID, wadau wa majukwaa ya Naweza, Sitetereki na waandishi wa habari wa mkoani hapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles