28.2 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mabadiliko Polisi

AGATHA CHARLES

RAIS Dk. John Magufuli, amefanya uteuzi na kuwapandisha vyeo maofisa watano wa Jeshi la Polisi kuwa Makamishna pamoja na kuwahamisha wengine wawili.

Katika mwelekeo huo huo, naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, amewahamisha baadhi ya maofisa na Makamanda wa Mikoa wa Jeshi la Polisi na kuwapandisha wengine.   

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Inspekta Jenerali wa Polisi, Sirro, alisema Rais ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, alimpandisha Naibu Kamishna wa Polisi, (DCP) Charles Mkumbo, kuwa Kamishna wa Polisi na kumteua kuongoza Kamisheni ya Polisi Intelijensia ya Jinai (CP Intel).

Alimtaja mwingine kuwa ni Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Liberatus Sabas, ambaye amepandishwa cheo na kuwa Kamishna wa Polisi na kuteuliwa kuongoza Kamisheni ya Polisi Operesheni na Mafunzo (CPO&T).

Pia Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Shaban Hiki, naye amepandishwa kuwa Kamishna wa Polisi ambaye ameteuliwa kuongoza Kamisheni ya Polisi Maabara ya Uchunguzi wa Kisayansi (CP F&B).

IGP Sirro, alisema Rais alimpandisha cheo Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Leonard Lwabuzala, kuwa Kamishna wa Polisi ambaye pia alimteua kuongoza Kamisheni ya Polisi Fedha na Lojistiki (CPF&L).

Mwingine ambaye Rais amempandisha cheo ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benedict Wakulyamba, ambaye amekuwa Kamishna wa Polisi, ataongoza Kamisheni ya Polisi Utawala na Menejimenti ya Utumishi (CPA&HRM).

Sirro aliwataja wengine wawili waliohamishwa kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambao ni Kamishna Albert Nyamhanga ambaye ameondolewa kutoka kuwa Kamishna wa Polisi Utawala na Menejimenti ya Utumishi na kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Idara ya Wakimbizi.

Alimtaja mwingine kuwa ni Kamishna Nsato Marijani ambaye anatoka kuwa Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Idara ya Wakimbizi.

Pamoja na hilo, IGP Sirro, ametangaza kufanya uhamisho wa baadhi ya makamanda wa mikoa ambapo aliyekuwa Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Gemini Mushi, anakwenda kuwa Mkufunzi Mkuu Chuo cha Polisi (CCP) Moshi.

Alisema Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Renata Mzinga ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Njombe, anakwenda Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam.

Ingawa IGP Sirro hakufafanua sababu zaidi za kuwahamisha makamanda hao akidai kuwa mabadiliko hayo yamefanyika ili kuongeza tija na kuboresha maeneo yanayolegalega hata hivyo kuamishwa kwa Renata kumekuja katika wakati ambao Mkoa aliokuwa akiuongoza ulikumbwa na mauaji ya watoto.

Katika mabadiliko hayo, IGP Sirro, amemhamisha aliyekuwa Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Simon Haule kwenda Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam.

“Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shana, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Arusha,” alisema Sirro.

Sirro alisema Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Amon Kakwale, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Kipolisi Temeke.

Mabadiliko hayo pia yamemgusa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Simon Maigwa, ambaye anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Ruvuma.

Kwa mujibu wa Sirro, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salum Hamduni, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Njombe kujaza nafasi ya Renata.

Aidha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Richard Abwao, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Shinyanga huku Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Zuber Chembera, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Kipolisi Ilala.

Pamoja na hayo, IGP Sirro, alisema hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari kwani uhalifu umepungua ukiwamo unyang’anyi wa kutumia silaha, biashara ya dawa za kulevya lakini bado changamoto iliyopo ni ubakaji.

“Matukio ya ubakaji yanaongezeka kutokana na mmomonyoko wa maadili. Tunajipanga kutoa elimu darasani tangu shule ya msingi na sekondari kwani wengi hawajui kama ni kosa. Tutatoa pia machapisho ya elimu kuhusu ubakaji,” alisema IGP Sirro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles