Na Mwandishi wetu
Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa ametangaza rasmi kurudi Chama Cha Mapinduzi(CCM) kuanzia leo Machi 1,2019.
Lowassa alihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenda upinzani katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) mwaka 2015.
Akiwa upinzani Lowassa aligombea urais lakini pia aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema
Akizungumza leo katika Ofisi za ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema ametafakari na kuamua kurudi nyumbani CCM ambako sehemu kubwa ya maisha yake imekuwa huko.
Wakati Lowassa anatangaza kurejea CCM alikuwa amesikindikizwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga ambaye pia aliwahi kuwa Mtunza fedha wa CCM Rostam Aziz.
Akiongea baada ya mapokezi hayo, Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amesema wamempokea Lowassa na katika kuthibitisha hilo waliona ni vema uamuzi wake akautangazia Ofisi za CCM Lumumba.
“Kwa upande wetu tumekaa, tumetafakari na kujiridhisha kuwa Lowassa amekaa kwenye Chama kwa muda mrefu na kwa bahati mbaya zilizojotokeza aliamua kwenda upinzani. Tumemsikiliza mawazo yake kwamba sehemu kubwa ya maisha yake ni kwenye Chama Cha Mapinduzi na kwamba kutokana na sababu ambazo amezieleza aliamua kwenda upinzani na leo hii amerudi nyumbani,”amesema Rais Magufuli.
Naye Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally amesema Lowassa amefikia uamuzi wa busara kwa kurudi nyumbani kwa ajili ya kushirikiana katika kuleta maendeleo ya wananchi wote.