Mwandishi wetu-Kibondo
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza ulinzi na doria katika maeneo ya mipaka kutokana na ongezeko la vitendo vya mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha.
Pia ameagiza wakimbizi wote watakaobainika kutoroka kambini na kuingia uraiani wakamatwe na kuchukuliwa hatua za sheria.
Majaliwa alisema hayo alipozungumza na wananchi kwenye Uwanja wa Taifa wilayani Kibondo wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kigoma.
Alisema maeneo yaliyo katika hali mbaya ni Kibondo, Buhigwe, Kasulu, Ngara, Biharamulo, Uvinza, Kakonko na Kigoma Vijijini, ambako wananchi hususan wafanyabiashara wameingiwa na hofu kutokana na vitendo hivyo.
Alisema pamoja na undugu waliokuwanao na nchi jirani, lakini kila nchi ina sheria na taratibu zake, hivyo ni lazima zifuatwe.
Alisema ni marufuku kuingia katika nchi yoyote bila ya kufuata sheria na taratibu za nchi husika.
“Kulinda usalama wa nchi ni jukumu letu sote na si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, kila mmoja anapaswa kushiriki.
“Kwa upande wa majirani zetu wanaotaka kuja nchini ni lazima wafuate taratibu kwa kuomba vibali,” alisema.
Alisema watu wote wanaoingia bila ya kufuata sheria na taratibu ndiyo hao wanashiriki katika vitendo vya uhalifu yakiwamo mauaji ya raia wasiokuwa na hatia, unyang’ani wa kutumia silaha za vita na utekaji wa watoto.
Waziri Mkuu alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kulinda mipaka ya nchi na watu wote watakaobainika wameingia nchini bila vibali wakamatwe na wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alisema wakimbizi wanaohifadhiwa katika maeneo mbalimbali nchini hawaruhusiwi kutoka nje ya kambi hizo kwa sababu huduma zote wanazostahili zikiwamo za afya, elimu na chakula zinapatikana kambini.
Pia Waziri Mkuu aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iwasimamie vizuri watumishi wake wanaofanya kazi kwenye kambi hizo na kuchukua hatua kwa watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Vilevile ameutaka uongozi wa wizara hiyo ufanye mazungumzo na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) litekeleze majukumu yake bila kukiuka sheria za nchi.