JUSTIN DAMIAN
KWA kipindi kirefu, kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika sekta ya fedha kama ukosefu wa utambulisho mahususi wa kuwatambua kirahisi wakopaji, ubora wa taarifa zao ambazo ni pamoja na usahihi, ukamilifu na upatikanaji katika muda mwafaka.
Uwepo wa wakopeshaji wasiosimamiwa na ambao hawalazimiki kutoa taarifa za mikopo za wateja wao na kukosekana kwa mwamko kuhusu suala la taarifa za mikopo pia imekuwa ni tatizo lingine.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na kampuni zinazoandaa taarifa za mikopo, mabenki, taasisi za fedha na wadau wengine wameamua kuchukua hatua za pamoja kutatua changamoto hizi na kutatua baadhi, huku nyingine zikiwa zinahitaji mchakato mrefu na muda wa kutosha kuweza kuzitatua.
Wiki iliyopita, BoT ilizindua kampeni ya kuelimisha umma kuhusu taarifa za mikopo na elimu ya fedha Tanzania tukio ambalo linatafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya uchumi na fedha kama hatua muhimu katika maendeleo ya sekta ya fedha nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga, alisema kuwa na mfumo mzuri wa taarifa za mikopo ni wajibu wa wadau wanne wakubwa ambao ni watoa mikopo, kampuni za kuandaa taarifa za mikopo, wakopaji (yaani watu binafsi/walaji na biashara) na mamlaka za udhibiti na usimamizi.
Alisema jitihada za wadau hawa wakubwa zinachangiwa na elimu ya fedha na kujenga mwamko miongoni mwa wakopaji/walaji na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa mfumo wa taarifa za mikopo kwa mtu binafsi, sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla.
“Elimu kuhusu masuala ya fedha ni muhimu katika mfumo mzima wa taarifa za mikopo. Kampeni hii ya elimu kwa umma inalenga kuwaelimisha watumiaji wa huduma za fedha na wadau wengine kukuza uelewa wao kuhusu taarifa za mikopo ili kuongeza ushiriki katika matumizi ya taarifa za mikopo hapa nchini.
Mpango huu ni sehemu ya mpango mpana zaidi wa kukuza elimu kuhusu masuala ya fedha kwa lengo la kukuza huduma jumuishi za kifedha Tanzania kutoka asilimia 65 mwaka 2018 hadi asilimia 75 ya watu wazima wanaotumia huduma za kifedha ifikapo mwaka 2022,” alifafanua.
Hivi sasa, kuna taasisi mbili zinazoandaa taarifa za mikopo ambazo zimesajiliwa na zinazofanya kazi hapa Tanzania. Taasisi hizo ni Dun & Bradstreet Credit Bureau Tanzania Limited na Creditinfo Tanzania Limited. Taasisi hizi hutayarisha taarifa hizo na kuzitoa kwa wakopeshaji na watumiaji wengine kwa ada fulani wanapozihitaji ili kuweza kujua hali ya kifedha ya watu wanaotaka kupata mikopo kutoka kwao.
Taasisi hizi zinapata taarifa zake kutoka kanzidata ambayo inasimamiwa na BoT na taarifa (data) nyingine kutoka taasisi zinazotoa huduma mbalimbali, kama kampuni za simu, wakala wa kukusanya madeni, wauzaji wa jumla na reja reja wanaotoa bidhaa na huduma kwa mkopo, taasisi za umma kama vile Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Masijala za Mahakama.
Awali, mabenki na taasisi za fedha zilikuwa zinachukua muda mrefu kuamua kukopesha na wakati mwingine zilifanya maamuzi ya kukopesha bila kuwa na taarifa sahihi za vihatarishi ambavyo vingeweza kusababishwa na maamuzi yao. Hali hii ilisababisha taasisi za fedha kukopesha kwa riba kubwa kutokana na kutokuwa na taarifa za mikopo za wakopaji na hivyo kuwa na vihatarishi vingi.
Mfumo wa taarifa za wakopaji utawawezesha wakopaji wenye historia nzuri ya ulipaji mikopo, kupata mikopo yenye riba nafuu ukilinganisha na wakopaji wasio na historia nzuri ya urejeshaji wa mikopo wanayochukua kwenye taasisi mbalimbali za fedha. Mfumo utawezesha wakopeshaji kupata taarifa kuhusu tabia za wakopaji ili kujua namna ya kuwahudumia ipasavyo kama wanahitaji mikopo.
“Kama kiwango cha kipimo (credit score) cha wakopaji ni kizuri, wanaweza kujadiliana na wakopeshaji ili kupata riba ndogo kwa mikopo hivyo kufanya mikopo iwe nafuu na ipatikane kwa urahisi. Taasisi za kuandaa taarifa za fedha pia zinasaidia uwajibikaji katika kukopesha na kuepusha wakopaji kuwa na madeni makubwa zaidi ya uwezo wao,” alisema.
Prof. Luoga, alisema kupeana taarifa za mikopo kunapunguza tofauti ya upatikanaji wa taarifa miongoni mwa wakopeshaji na wakopaji na kupunguza gharama za kutafuta taarifa hizo na hivyo kuboresha upatikanaji wa mikopo kwa sehemu kubwa ya wananchi na kuongeza kuwa taarifa hizo zinasaidia kupanga bei kwa kuzingatia vihatarishi, hali ambayo inaweza kupunguza gharama kwa wakopaji/walaji wenye historia nzuri ya ukopaji kwa kupata mikopo kwa masharti na viwango vya riba nafuu.
“BoT inaona matumizi ya mfumo wa taarifa za mikopo utasaidia katika kuchambua jinsi taasisi za ukopeshaji zinavyosimamia vihatarishi katika mikopo na kwamba itakuwa ikifuatilia kuhakikisha kwamba mikopo inatolewa kwa kuzingatia mfumo huo na taarifa nyingine katika kusimamia vihatarishi vya mikopo,” alisema.
Gavana Luoga aliongeza kuwa kushirikishana taarifa za mikopo kunachangia katika kujenga nidhamu ya ukopaji kwa kuepuka kukopa bila sababu na kuchukua mikopo mikubwa na kwa wakopeshaji, taarifa za mikopo zinarahisisha kuangalia vihatarishi na kufanya maamuzi bora wakati wa kutoa mikopo kwa taasisi na wajasiriamali wadogo pamoja na kufuatilia wakopaji kwa ufanisi zaidi.