28.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mbio Uchaguzi Mkuu 2020 zaanza

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MBIO za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, sasa zimeanza baada ya Serikali kutangaza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ipo kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.

Mara ya mwisho kuboreshwa daftari la kudumu la wapigakura ni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ambao Rais John Magufuli alitangazwa mshindi na NEC kwa kupata kura 8,882,935 ikiwa ni asilimia 58.46.

Mpinzani wake wa karibu Edward Lowassa aliyekuwa akipeperusha bandera ya Chadema chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alitangazwa kupata kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote.

Jana bungeni, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso (Chadema), alisema uboreshaji wa daftari hilo uko mbioni.

Katika swali lake, Pareso alidai kuwa umebaki mwaka mmoja, kuelekea uchaguzi Mkuu mwaka 2020 ili Watanzania waliokidhi vigezo wapate haki ya kupiga kura.

“Je, lini Serikali itaanzisha mchakato wa kuboresha daftari la wapigakura?” aliuliza Pareso.

Akijibu swali hilo, Mavunde alisema kwa mujibu wa kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Uchaguzi, sura ya 343, NEC ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa mara ya kwanza na uandikishaji wa majaribio kwa baadhi ya mikoa.

Mavunde alisema mchakato wa kuboresha daftari hilo ulianza Agosti mwaka jana kwa kufanya maandalizi ya kuhuisha kanzi data ya daftari hilo pamoja na kuboresha mifumo ya uandikishaji na utunzaji wa kumbukumbu.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, watu waliokuwa wamejiandikisha kupiga kura walikuwa 23,161,440 lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa 15,589,639 sawa na  asilimia 67.31 ya wapigakura wote.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, idadi ya wapigakura waliojiandikisha walikuwa 20,137,303, lakini waliopiga kura Oktoba 31 mwaka huo walikuwa 8,626,283 sawa na asilimia 42.84 ya wapigakura wote waliojiandikisha.

Takwimu hizi zimetolewa katika ngazi ya mkoa, wilaya, jimbo la uchaguzi na kata au shehia kama ilivyokuwa mwaka 2010. Makadirio ya idadi ya wapigakura yametokana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Kwa mujibu wa ripoti iliyo kwenye kitabu maalumu cha takwimu za wapigakura mwaka huu, ambayo nakala yake imepatikana kupitia Ofisi ya Takwimu ya Mkoa wa Arusha, idadi hiyo imepatikana kwa kutumia mbinu za kidemografia zinazohusisha mabadiliko katika viwango vya uzazi, vifo, uhamaji na uhamiaji katika ngazi ya taifa, mkoa, wilaya, majimbo ya uchaguzi na kata au shehia husika.

Ilikuwa ikikadiriwa kuwa ifikapo siku ya uchaguzi, Tanzania ingekuwa na watu wapatao 48,522,229 na watakaokuwa na umri wa kupiga kura watakuwa 24,252,927 iwapo wote watafanikiwa kuandikishwa upya.

Daftari la kudumu la wapigakura lilianzishwa chini ya ibara ya 5 (3) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, iliyolipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria ya kuanzisha daftari hilo na kuweka utaratibu wa kurekebisha yaliyomo.

Vifungu vya 11, 12 na 15 (5) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 na kifungu cha 15 B cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa sura ya 292 pia vinaeleza kuhusu daftari la kudumu la wapigakura.

NEC hutekeleza jukumu la uboreshaji au uandikishaji wa wapigakura chini ya ibara ya 74 (6) (a) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kupitia ibara hiyo, NEC inawajibika kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapigakura wapya waliotimiza umri wa kuandikishwa kwa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.

Kwa kuzingatia kifungu cha 15 (5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343, NEC inatakiwa kuboresha daftari la kudumu la wapigakura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na unaofuata.

NEC ilianzisha daftari la kudumu la wapigakura kwa mara ya kwanza mwaka 2004 kwa lengo la kuandikisha kila raia mwenye sifa za kupiga kura na kutunza taarifa zake katika daftari hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles