BOLLEN NGETTI
BARA la Afrika na Waafrika wamepitia enzi mbalimbali hadi kugota hapa. Waafrika wamewahi kujitawala wakiishi kwa uhuru kabla ya kuvamiwa na wakoloni weupe na kufanywa watumwa huku wengine wakiuzwa kwa kupigwa bei sawa na mbuzi wa shughuli mnadani.
Hata hivyo, Waafrika hao hao walipambana kufa na kupona dhidi ya wakoloni wakongwe na ilipofika kati ya miaka ya 1959 baadhi ya nchi zilianza kujitwalia uhuru ikianza na Ghana ya Kwame Nkuruma. Hakika kilikuwa ni kipindi cha vita iliyogharimu nguvu, jasho na damu lakini pia diplomasia iliyopevuka kama ilivyotokea kwa Hayati Mwalimu Nyerere wa Tanganyika 1961.
Historia inatuonesha kuwa baada ya uhuru nchi nyingi za Afrika zilijikuta katika mapambano mapya. Safari hii ikawa ni mapambano ya kugombea madaraka baada ya viongozi wake badala ya kuongoza wananchi wao walijigeuza kuwa wakoloni weusi, miungu watu na madikteta ambao hawakuhitaji kukosolewa maana wengi waliamini kuwa kiongozi kunaongeza uwezo wa akili na kufikiri na hivyo unapokuwa kiongozi basi wewe ndiye mwenye akili kuliko wananchi wako wote na unatakiwa hata kufikiri kwa niaba yao.
Kwa kuwa wanadamu ni viumbe tofauti na wanyama hayawani wanaoweza kunyamazishwa kwa viboko, vitisho na mikwara kukaanza kutokea maasi na Mapinduzi ya Kijeshi Afrika. Hata Tanzania Mwalimu Nyerere alishuhudia uasi wa askari wake jaribio ambalo hata hivyo lilizimwa kabla ya kutekelezwa!
Katika baadhi ya nchi za Afrika hali ilikuwa ni mbaya sana maana Mapinduzi hayo yalisababisha umwagaji mkubwa wa damu, watu kutekwa, kuteswa, kupotea na kuuliwa. Kwa hakika miaka ya 80’ na 90 kilikuwa ni kipindi kigumu mno kwa Afrika. Kinachotia mashaka ni kuona adui mkubwa wa Afrika na Waafrika ni Waafrika wenyewe kiasi cha Donald Trump kusema, “Afrika haijaweza kujitawala, watawaliwe tena.”
Ni kauli iliyoibua hasira miongoni mwa baadhi ya Waafrika na viongozi wao lakini kiukweli unaweza kuona uhalisia wa kauli ya Trump. Ukweli siku zote unauma sana!
Baada ya ukoloni mkongwe, baada ya Mapinduzi ya kila mara, sasa jinamizi jipya linaonekana kulivamia Bara la Afrika na Waafrika wenyewe. Ninazungumzia ujio wa mitandao ya kijamii na intaneti (social media).
Dunia inapiga hatua kwa haraka sana katika sekta ya mawasiliano na habari hususani intaneti. Dunia sasa ni kijiji ambapo unaweza kulizunguka kwa muda mchache kutoka mwanzo wa kijiji hicho hadi mwisho. Dunia sasa iko kiganjani mwa mwanakijiji. Leo ndani ya sekunde kadhaa unaweza kujua nini kinatokea Washington DC, Paris, Cairo, Bujumbura na kwa wakati huo huo ukajua kinachoendelea uwanja wa Nang’wanda-Lindi, Kaliua-Tabora na Katerero Kagera kwa wakati mmoja.
Mbali na mawasiliano ya simu, sasa tuna mitandao kama WhatsApp, Facebook, Instagram, SmartChat, IMO, Tweeter nakadhalika. Mitandao hii imerahisisha mno mawasiliano kwa haraka jambo ambalo sasa ni tishio kwa vyombo vya habari rasmi kama redio, televisheni na magazeti ambayo habari zake ni lazima kupitia mikononi mwa wahariri kabla ya kuwafikia wasikilizaji, watazamaji na wasomaji. Sasa kila mtu mwenye kumiliki simu janja (smart phone) ni mwanahabari huru ili kukamilisha maana halisi ya “social media”.
Sasa tunashuhudia kila inapokaribia kampeni za uchaguzi na uchaguzi wenyewe barani Afrika watawala huhangaika na mitandao ya kijamii kwa hofu tu ya upashanaji habari. Nchini Uganda siku mbili kabla ya uchaguzi uliomweka Rais Yoweri Museveni madarakani intaneti na mitandao ya kijamii kwa ujumla ilizimwa nchi nzima kwa hofu tu ya kupashana habari za matokeo ya uchaguzi huo.
Hapa dhana nzima ya uhuru wa kutoa maoni na mawazo ukabinywa na kunyongwa. Huko Sudan ambako sasa hakujatulia wananchi wakitumia haki yao ya kikatiba kuandamana kupinga kupanda kwa gharama na bei ya vitu kama mkate na mafuta Serikali hiyo imeamua kuzima mitandao ya kijamii ili tu watu wasipashane habari.
Hali ni hiyo hiyo huko DRC (Kongo) katika uchaguzi unaomsukuma Joseph Kabila pembeni Serikali imezima intaneti na mitandao yote ya kijamii ili kusiwepo na upashanaji habari. Hali ni hiyo hiyo nchini Burundi na Rwanda ambako matumizi ya mitandao ni kujitakia jela. Ukijaribu kusoma hoja za watawala kuhusu mitandao hii ni hofu tu ya kuumbuliwa kwa maovu wanayoficha isijulikane na umma mpana.
Huko Marekani tulishuhudia namna Donald Trump alivyotumia mtandao wa Tweeter kwa asilimia 57 kufanya kampeni na hatimaye kushinda uchaguzi. Hii yote ni kuonesha nguvu ya mitandao ya kijamii ambayo watumiaji wake kwa sehemu kubwa ni vijana walio chini ya miaka 35.
Rai yangu kwa makampuni yanayomiliki mitandao hii kutokubali kwa mitandao yao kuzimwa maana ikumbukwe si wote wanaotoa taarifa zinazowachukiza watawala na badala yake hutumia mitandao hii kufanya biashara na hivyo kuzima mitandao ni hatua isiyo na tija yoyote. Wananchi waelimishwe tu namna ya kutumia mitandao hii ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi kwa wakati sahihi isiyohatarisha usalama wa nchi.
Na hapa ninavutiwa na mtandao wa WhatsApp ambao hakuna anayeweza kuingilia isipokuwa wenyewe walioko nchini Marekani. Unadaiwa kuwa mtandao ulio salama zaidi kwa sasa!
Ni vizuri sasa wamiliki wa mitandao mingine kuona haja ya watumiaji wao wasitegemee vyombo hivi vya Afrika vilivyojaa ukiritimba, ubabe na ushirikina (regulatory authorities) ili watumiaji watoe maoni yao kwa uhuru. Kwa mfano Tanzania, TCRA ifanye kazi ya kuelimisha umma namna bora ya kutumia mitandao ya kijamii bila kuingilia uhuru wao.
Hata kwenye anga, tunalo anga la Tanzania lakini pia tunalo anga la Kimataifa ambalo kama Tanzania licha ya ndege kupita juu ya ardhi yetu lakini hatuna mamlaka nalo. Ingependeza pia katika suala la kudhibiti mitandao ya kijamii kuwe na utaratibu huu ili kupambana na watawala waoga wasiopenda kuona demokrasia ikichanua Afrika kama ilivyo Uropa na kwingineko. Hoja yangu ni haki na uhuru wa binadamu wa kutoa maoni yake bila kujificha kwenye hoja dhaifu ya, “uhuru una mipaka” lakini ukiangalia mipaka inayowekwa na watawala wa Afrika ni ushirikina na ubazazi usio na tija yoyote zaidi ya kuleta mitafaruku, migongano, chuki, mitulinga na umasiki!
Mwandishi ni mchambuzi habari za siasa na maendeleo ya jamii. Anapatikana kwa simu namba 0763 014452