KINSHASA, DRC
MAHAKAMA ya Katiba katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) jana ilianza kusikiliza ombi la kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi kiongozi wa upinzani, Felix Tshisekedi.
Ombi hilo limewasilishwa na mgombea mwingine wa upinzani, Martin Fayulu, aliyetangazwa kushika nafasi ya pili kwenye uchaguzi huo uliofanyika Desemba 30, mwaka jana utakaoshuhudia kiongozi mpya akimrithi Rais Joseph Kabila.
Fayulu ameyaita matokeo hayo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (CENI) kuwa ni mapinduzi ya uchaguzi.
Tshisekedi alitangazwa kupata asimilia 38.57 ya kura dhidi ya asilimia 34.8 za Fayulu.
Kwa mujibu wa CENI, mgombea aliyekuwa akiungwa mkono na Kabila alishika nafasi ya tatu akiwa na asilimia 23.8.
Hata hivyo, akitegemea matokeo yanayosemekana kukusanywa na mawakala wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (CENCO), Fayulu anasema ni yeye aliyechaguliwa kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura.
Mahakama ya Katiba ina wiki moja ya kuamua juu ya madai ya Fayulu.