RENATHA KIPAKA, BUKOBA
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora amesema pamoja na kuwa na majukumu mengi ya kusimamia, suala la utapiamulo ndani ya mkoa huo ni miongoni mwa mambo hatarishi yanayopaswa kushughulikiwa kuongeza uwezo wa kufikiri watoto na kizazi kijacho.
Alitoa kauli hiyo juzi alipokutana na watumishi wa ofisi yake ikiwa ni siku chache baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Alisema yuko mkoani humo kuleta mabadiliko ya maendeleo, uchumi, afya na fikra.
Profesa Kamuzora alitaja kipaumbele chake ni kuona namna bora ya kupambana na suala la utapiamlo hasa kwa watoto.
Alisema hiyo ni kwa kuzingatia takwimu zunazoonyesha Mkoa wa Kagera unashika nafasi ya nne kwa asilimia 41.7 kati ya mikoa 25 Tanzania Bara.
Alisema takwimu hizo zinatisha na si rafiki katika ustawi wa jamii kwa sababu zinatengeneza kizazi chenye udumavu hasa wa akili kwa watoto ambao ndiyo taifa la kesho.
“Kama hatutaangaika na suala hili la utapiamlo hatuwezi kusonga mbele kwa sababu hata uwezo wa kufikiri hasa kwa watoto wetu ni mdogo utaendelea kuwa mdogo jambo ambalo ni hatari kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Mkoa wa Kagera unakabiliwa na tatizo kubwa la utapiamlo ambako unashika nafasi ya nne kutoka mwisho ukiwa na asilimia 41.7.