NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KLABU ya Yanga jana imeingia mkataba wa miaka miwili na mshambuliaji Mbrazil, Geilson Santos Santana ‘Jaja’, kuichezea timu hiyo, ambapo mkataba huo utafikia kikomo mwaka 2016.
Jaja alijiunga na kikosi hicho wiki iliyopita ambapo alianza kupewa mazoezi ya peke yake kwa ajili ya kumfanya azoee hali ya hewa, huku wakiwa katika uangalizi wa kiwango chake kabla ya kupewa mkataba huo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, alisema usajili huo wa Jaja unaifanya timu hiyo kuwa na wachezaji wawili wa kimataifa waliowasajili msimu huu, wote wakitokea nchini Brazil, akiwemo Andrey Coutinho.
“Kazi yetu uongozi ni kutekeleza maelekezo ya kocha mkuu pamoja na benchi la ufundi, walitoa mapendekezo ya usajili kabla hawajaanza kazi na mengine baada kuwasili, yote tunajitahidi kuyatekeleza ili kila kitu kiende safi,” alisema.
Alisema mchezaji huyo ataanza kuitumikia timu kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika (CECAFA), inayotarajia kuanza Agosti 8 nchini Rwanda, kabla hawajaanza Ligi Kuu Septemba 20.
Alisema, Jaja alizaliwa Septemba 21 mwaka 1985 na kukulia katika mji wa Aracaju, nchini Brazil, mpaka anasajiliwa na timu ya Young Africans alikuwa akiichezea timu ya Itabaina FC iliyopo nchini Brazil.
Yanga 2nataraji makubwa zaid kutokana na maandaliz.Kila la kher YANGA na WADAU wooote