RIYADH, SAUDI ARABIA
MAHAKAMA nchini Saudi Arabia, imeanza kusikiliza kesi ya watu 11 walioshtakiwa kwa kuhusika na mauaji ya mwanahabari, Jamal Khashoggi, miezi mitatu iliyopita.
Mwendesha mashtaka mkuu wa nchi hiyo, Saud al-Mojeb, jana ameliambia Shirika la Habari la Serikali, SPA kuwa washtakiwa hao 11 ambao wote ni raia wa Saudia walifikishwa katika Mahakama ya Uhalifu mjini Riyadh kwa ajili ya kusikilizwa kesi yao kwa mara ya kwanza.
Taarifa hiyo imesema miongoni mwao ni watuhumiwa watano ambao waendesha mashtaka wanataka wapewe adhabu ya kifo kutokana na kuhusika moja kwa moja na mauaji ya Khashoggi.
Khashoggi, mkosoaji mkubwa wa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohamemd bin Salman, aliuawa Oktoba 2 mwaka jana baada ya kuingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul nchini Uturuki, tukio ambalo lilizusha shutuma za kimataifa. Hata hivyo, hakuna tarehe iliyopangwa kwa ajili ya kikao kijacho cha kusikilizwa kesi hiyo.