29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Watanzania tusidekezwe na utafiti

g4*Asema hawezi kuwa rais bila kupigiwa kura

*Aanza kurusha makombora Ukawa

Na Bakari Kimwanga, Kahama

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewataka Watanzania kutodekezwa na matokeo ya utafiti unaoendelea kutolewa na taasisi mbalimbali.

 

Kauli hiyo aliitoa jana kwa nyakati tofauti, alipohutubia mikutano ya kampeni iliyofanyika katika majimbo ya Busanda, Mbogwe ya mkoani Geita na majimbo ya Ushetu na Kahama Mjini ya mkoani Shinyanga.

 

Alisema katu utafiti huo hauwezi kumfanya awe rais na hivyo ni lazima wana CCM na Watanzania kwa ujumla wampigie kura nyingi za ndiyo ili ashinde kwa asilimia 95.

 

Pia aliwataka wanachama wa CCM kutobweteka kwa kuwahamasisha watu kwenda kupiga kura.

 

“CCM na Watanzania tusidekezwe na utafiti, nataka kushinda kwa asilimia 95, nendeni mkapige kura, maana sasa watakuja watu na kuwaambia tumeshinda kwa utafiti.

“Hapana, siwezi kushinda kwa maneno, Oktoba 25 nendeni asubuhi na mkapige kura kwa wingi kwa kuweka alama ya vema katika picha ya Magufuli na pigeni kura kwa amani na utulivu, kwangu ni kazi tu,” alisema Dk. Magufuli.

 

Msimamo huo alioutoa umekuja siku chache baada ya Taasisi ya Twaweza kutoa matokeo ya utafiti na kueleza kuwa mgombea huyo wa urais anaweza kushinda kwa asilimia 65, akifuatiwa na mgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa, angepata asilimia 25.

Taasisi nyingine ya Utafiti ya Ipsos ilitoa matokeo yake juzi na kusema Dk. Magufuli angeshinda urais kwa asilimia 62 (kama uchaguzi ungefanyika juzi), huku Lowassa angepata asilimia 31.

ILANI NA KERO YA MAJI

Akizungumza na wananchi wa Nyarugusu, Dk. Magufuli, alisema anajua changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.

Kutokana na hali hiyo, amejipanga kutatua kero hiyo kwa kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeeleza kwa maeneo ya vijijini maji yatapelekwa kwa asilimia 75 na mijini asilimia 95.

Alisema haiwezekani maeneo yanayozalisha madini ambayo pia huchangia pato la Taifa kukosa maji ya uhakika.

“Ilani ya uchaguzi ya CCM imeeleza vizuri sana na mipango yetu kuanzia mwaka kesho tutasambaza maji kwa asilimia 75 vijijini na mijini asilimia 95. Lakini pia ninajua hapa kuna wachimbaji wadogo ambao wanahitaji maeneo ya kuchimba dhahabu yao.

“Sawa tutalinda maslahi ya wachimbaji, lakini si wakubwa peke yao, hata wadogo pia tutawapa maeneo yao ili nao wafaidi rasilimali za nchi yao kama CCM inavyotaka,” alisema Magufuli.

 

Alitaka Watanzania waendelee kumwamini kwa kuwa amejipanga kutatua kero zao kwa vitendo.

Alisema hawezi kutoa ahadi za uongo kwa Watanzania ambazo hazitekelezeki, ikiwemo ya kuondoa nyumba za tembe ila atakachokifanya ni kuhakikisha Serikali yake inapunguza bei ya vifaa vya ujenzi ili wananchi wajenge nyumba nzuri na za kisasa.

 

Alisema anatambua Watanzania wanahitaji mabadiliko ya kweli katika nchi yao na yatapatikana chini ya Serikali yake.

 

KOMBORA UKAWA

Mgombea huyo wa urais alisema anashangazwa na baadhi ya wanasiasa aliowataja majina kwa mara ya kwanza, hasa Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, wanaodai CCM haijafanya kitu.

Alisema viongozi hao pamoja na kuwahi kuwa katika nafasi za juu serikalini, lakini wameshindwa kutambua hata baadhi ya huduma walizosimamia wenyewe.

“CCM si malaika, ila kuna watu ambao si wazuri na wengine wameondoka, je, Lowassa, Sumaye, Mgeja (Khamis) wote walikuwa CCM, sasa leo wanasema hakuna kilichofanyika, kama wameshindwa wakiwa katika nafasi ya uwaziri mkuu, je wakipewa nchi?

 

“Ninaomba mniamini mimi ndiye Magufuli, nimejipanga kutatua kero za Watanzania wote bila kujali itikadi zao za vyama, wanasema Serikali ya CCM imechoka, ila ni wao ndiyo wameifanya ichoke kwa kuifikisha hapa ilipo.

 

“Wao walikuwa na madaraka makubwa kwa kuwa unapokuwa waziri mkuu ndiyo mshauri mkuu wa rais, mimi sijawahi kuwa na madaraka makubwa, sasa nataka kuwatumikia Watanzania,” alisema Dk. Magufuli.

 

SITTA AMSIKITIKIA LEMBELI

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni za CCM Taifa, Samuel Sitta, amesikitikia kitendo cha rafiki yake, James Lembeli kukimbia CCM na kujiunga na Chadema.

Alisema Lembeli alikuwa ni mmoja wa wabunge waliojipambanua kupinga maovu, ikiwemo ufisadi, lakini naye ameshindwa kuhimili vishindo na kuamua kuondoka.

“Hapa Kahama kuna ndugu yetu James Lembeli ambaye alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa wanapinga maovu, leo naye ameungana na wale wenzie kule.

 

“Si ajabu kama amekwenda huko naye lakini nauliza yale aliyokuwa anayasimamia ataweza? Pia ninawaomba sana majimbo yote ya Mkoa wa Shinyanga tunataka yawe chini ya mikono ya CCM na ninawaomba mniunge mkono,” alisema.

 

Sitta, aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la tisa na kwa sasa ni Waziri wa Uchukuzi, aliwataka wananchi wa Kahama kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kumpigia kura Dk. Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Jumanne Kishimba.

 

Awali, kabla ya Dk. Magufuli hajaanza kuhutubia, mkuu wa msafara za mgombea urais, Abdallah Bulembo, aliwataka wananchi waliofurika katika uwanja wa mkutano kumkumbuka aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma), Celina Kombani, aliyefariki dunia juzi nchini India

Baada ya dua hiyo, Bulembo alisema anashangazwa na kitendo cha Lembeli badala ya kugombea ubunge kwao Ushetu ametafuta kivuli cha kujifichia Kahama Mjini.

 

“Leo (jana) tumetoka Ushetu ambapo ni kwao, kule wamesema pamoja na kuwa kwake, lakini asingepata kura, sasa nanyi hapa Kahama Mjini mnyimeni kura.

“Alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili amewafukuzisha kazi watu na hata kuonekana ni mtu mwenye heshima na ninapata tabu na watu wenye nywele nyeupe kama Lembeli,” alisema Bulembo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles