MWANDISHI WETU – Dar es Salaam
WAKATI vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vikitarajiwa kuanza kuketi kesho na kesho kutwa jijini Dar es Salaam, mambo kadhaa huenda yakatawala ikiwamo hali yakisiasa na kuitwa kuhojiwa kuhusu harakati zake za urais mwaka 2020 kada wachama hicho, Bernard Membe.
Hata hivyo taarifa kutoka kwa baadhi ya wana CCM zinaeleza kuwa agenda za vikao hivyo vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ambavyo kwa kawaida huketi na kujadili pamoja na kupitisha masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya chama hicho bado hazijawekwa wazi.
Pamoja na hali hiyo, ukiacha suala la hali ya kisiasa na lile la Membe lililotikisa hivi karibuni, wengi wanabashiri pia mwenendo wa uchaguzi wa Serikali za mitaamwakani na ule wa 2020 bara na visiwani, lakini pia matamko mbalimbali ndani ya nje ya nchi na mali za CCM huenda yakajadiliwa.
Taarifa ambazo MTANZANIA Jumapili limezipata kupitia vyanzo tofauti zilidai kuwa vikao hivyo vitafanyika Dar es Salaam na vitaongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, RaisDk. John Magufuli.
Jitihada zagazeti hili kuwapata Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally pamoja na Katibuwa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole ili kuzungumzia ajenda za mkutano huo ziligonga mwamba baada ya kudaiwa kuwa walikuwa katika vikao vilivyokuwa vikiendelea.
Pamoja najitihada za kuwatafuta viongozi hao kwa simu kushindikana, juzi na jana gazetihili lilifika ofisi za CCM- Lumumba na kujibiwa kuwa Katibu Mkuu alikuwa katika vikao vya kawaida vya chama.
Kada mmojawa CCM kutoka Jumuiya ya Vijana aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kuhifadhiwa jina lake alisema ingawa agenda hazijawekwa wazi lakiniwana CCM wengi wanadhani suala la Membe na wengine wanaotuhumiwa kukihujumu CCM kuelekea 2020 wakajadiliwa.
Hivi karibuni suala la Membe lilitawala vichwa vya habari baada ya Katibu Mkuu , Dk. Bashiru kumuita ajieleze kwa tuhuma za kumuhujumu Rais Magufuli kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Jibu laMembe ambaye amepata kuwania kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM mwaka 2015kwa Dk. Bashiru akitaka mtu anaye mtuhumu naye awepo katika kikao hicho ndilo lililoibua mabishano na hata mijadala ndani na nje ya CCM.
Hadi sasaMembe na Dk. Bashiru hawajakutana hali ambayo imejenga hisia kwamba huenda katika vikao hivyo akaitwa au suala lake likajadiliwa.
Mbali nahilo Wadadisi wa mambo wanadai pamoja na mambo mengine huenda suala la mali za chama hicho litajadiliwa kwa kutazama wale waliorejesha na ambao bado.
Hilo linachagizwa na kauli ya Novemba mwaka huu aliyoitoa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Anna Abdallah kuwa kutafanyika uhakiki mwingine nchi nzima.
Kauli hiyo ambayo aliitoa kupitia gazeti hili, alisema uhakiki wa ripoti ya kwanza ya Tumeya Dk. Bashiru haikuweza kuzifikia mali zote za chama hicho.
Hatua hiyo ilikuja ikiwa imepita takribani miezi sita tangu ripoti ya Tume ya uhakiki wa mali za CCM iliyokuwa ikiongozwa na Dk. Bashiru, kukabidhiwa kwa Rais Magufuli.
Kamati hiyo ilichukua muda wa miezi mitano kukamilisha kazi hiyo kwa kukusanya taarifa,kuhakiki na kuchambua nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama hicho.
Pia iliangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wake,ilikusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na namna yakusimamia mali hizo.