KLABU ya Barcelona itashindwa kushiriki michuano ya Ligi Kuu nchini Hispania endapo Catalonia itafanikiwa kupata uhuru na kujitenga na Hispania.
Mikoa mbalimbali ya Catalonia inatarajia kupiga kura Septemba 27, mwaka huu kwa ajili ya kujitenga na nchi ya Hispania.
Rais wa Shirikisho la Soka nchini Hispania, Javier Tebas, amesema endapo Catalonia itafanikiwa kuwa huru, basi
klabu ya Barcelona itaondolewa kwenye michuano ya Ligi Kuu nchini humo.
“Mgawanyiko wa Catalonia na Hispania utasababisha kupoteza ubora wa soka la nchini Hispania, kwa kuwa kama Catalonia
itafanikiwa kuwa huru, basi Barcelona
watakuwa hawahusiki na michuano ya La
Liga.
“Itabidi iwe hivyo, ni bora hali hii ikatulia, lakini vinginevyo itasababisha kupoteza ubora wa soka,” alisema Tebas.
Hata hivyo, Waziri wa michezo nchini humo, Miguel Cardenal, amesema kama Catalonia itafanikiwa kuwa huru, basi
Barcelona itatolewa katika michuano ya klabu za bara la Ulaya.
“Catalonia itaifanya Barcelona kupoteza idadi kubwa ya mashabiki duniani na itapunguza kipato kwa kuwa mashabiki wao duniani wataanza kupungua.
“Kutokana na hali hiyo, timu ya Barcelona itakuwa ni timu ya kawaida kama ilivyo kwa klabu ya Ajax, Celtic au Standard Liege,” alisema Cardenal.
Hata hivyo, mashabiki wa Barcelona wanaamini kuwa endapo Catalonia itafanikiwa kuwa huru, bado klabu hiyo ina
nafasi ya kuendelea kushiriki Ligi hiyo.