ANDREW MSECHU
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeiomba Mahakama ya Rufani kuharakisha kusikiliza rufani inayohusu kuondolewa kwa dhamana ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko ambao wanaendelea kusota rumande kwa siku 13 sasa.
Ombi hilo lilitolewa na Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika jana ambaye alieleza kuwa chama hicho kinaamini Mahakama ya Rufaa ina uwezo wa kuitisha na kupitia majalada yote yanayohusu rekodi ya mwenendo wa shauri hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa haraka ili kutoa haki.
Mnyika alisema anaamini Mahakama ya Rufaa ambayo ilionyesha nia ya kushughulikia suala hilo kwa haraka tangu hatua ya awali, kukamilisha kutolea uamuzi wa shauri hilo kabla mahakama haijaenda likizo Desemba 15.
“Tunajua majaji wengi wa Mahakama ya Rufaa wako mikoani kwa ajili ya kushughulikia mashauri kwa mujibu wa ratiba yao. Sisi tuko tayari kumfuata Jaji popote alipo hata kama ikiwa mikoani ili tu suala hili la kufutwa kwa dhamana ya Mbowe na Matiko lishughulikiwe kwa wakati na haki isicheleweshwe,” alisema.
Aliema anaamini pia kuwa wanasheria wa Serikali ambao wamekuwa wakijaribu kutafuta njia za kukwamisha au kuchelewesha kusikilizwa rufani hiyo, wana uwezo wa kuamua kuondoa notisi iliyowekwa mahakamani ambayo wanaamini ina lengo la kuchelewesha muda wa mahakama na kusababisha matumizi mabaya ya rasilimali za mahakama.
“Tunajua uamuzi wa Mahakama ya Rufani unaweza kuziita pande zote mbili kwa dharura na kwa haraka kama ambavyo Mahakama Kuu ilifanya awali katika suala hili na hii itasaidia kuwafanya wale wa upande wa mashtaka ambao wananuia kuyumbisha mchakato wa utoaji haki wakose la kufanya,” alisisitiza.
Wito kwa Serikali
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba (Chadema) alitoa wito kwa Rais John Magufuli, Waziri wa Sheria Profesa Palamagamba Kabudi, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuonyesha Serikali haina mkono wake katika suala hilo kwa kuwaeleza waendesha mashtaka kuheshimu sheria na kuacha kupoteza muda.
“Tunajua chanzo cha kesi hii ni uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni wakati tulipokuwa tukidai haki ya mawakala wetu kupata hati za kiapo ambazo walikuwa hawajapewa hadi dakika za mwisho.
“Polisi walitumia nguvu na kusababisha mauaji ya mwanafunzi Akwilina (Akwilini, Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji, (NIT), aliyefariki dunia kwa kupigwa risasi) leo tunaona badala ya wauaji kushughulikiwa, viongozi wetu ndiyo waliobambikizwa kesi kwa madai ya kusababisha mauaji huku wauaji wakiachiwa.
“Kwa kuwa kesi hii chanzo chake ni uchaguzi, tunahitaji kuona haki ikitendeka na suala sasa liwe ni mjadala wa umma kuhusu tume huru ya uchaguzi na kuelekea kwenye mkondo sahihi wa uchaguzi huru na wa haki tunapoelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020, siyo kuishia kupigania haki mahakamani katika masuala ambayo ni ya kubambikizwa,” alisema.
Alisisitiza viongozi hao wakuu wa Serikali wanatakiwa kuonyesha umma kuwa hawahusiki katika kupandikiza kesi hizo kwa nia ya kufunika tuhuma za mauaji ya Akwilina na kubadili mjadala kutoka mauaji hadi kutafuta haki mahakamani na sasa hivi kutoa mwelekeo wa mjadala wa Mbowe na Matiko kufutiwa dhamana katika kesi yenye masharti ya dhamana yasiyoeleweka.
Wito kwa wanachama
Mnyika alisema kwa kuwa kesi hiyo ya msingi ya viongozi wa Chadema inatajwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ujumbe wa Mwenyekiti wao, Mbowe ni kwamba wanatakiwa wasimlilie yeye bali watumie fursa ya kuwekwa kwao ndani kulilia taifa kwa kupigania mabadiliko mapya ya tume huru ya uchaguzi kwa kuwa msingi wa kesi yao ni uchaguzi.
Alisema kwa kuwa leo ni siku ambayo Mbowe na Matiko watapelekwa tena mahakamani, wanachama popote walipo wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kuwafariji viongozi hao na kutumia fursa zote walizo nazo kwa kufika mahakamani na kutumia mitandao ya jamii kuwasilisha ujumbe wa kupinga hujuma dhidi ya viongozi wao.
“Tunajua chumba cha mahakama ni kidogo, lakini eneo la mahakama ni kubwa. Kwa wale ambao hawatapata nafasi kwenye eneo la mahakama hata kama wakisimama barabarani wataonyesha nia ya kuwafariji viongozi wetu. Kwa wale ambao watashindwa kufika mahakamani, wakiwa Dar es Salaam au mikoani, watumie fursa ya mitandao ya jamii kuonyesha kwamba hawakubaliani na jambo hili,” alisema.
Aliwataka pia wabunge waliopo kwenye michezo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayoendelea Burundi kutumia nafasi yao kuonyesha kutokubaliana na hatua hiyo kwa kuwa Matiko alipewa barua na kutumwa na Bunge kw ajili ya kuandaa mazingira ya wabunge hao kufika salama kwenye michezo hiyo lakini mahakama ilishindwa kuheshimu na hata Spika wa Bunge ameshindwa kuheshimu muhimili anaouongoza kwa kukaa kimya wakati wabunge wakidhalilshwa.