31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tucta yataka Serikali kurudi mezani mafao ya wafanyakazi

ASHURA KAZINJA-MOROGORO



SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeiomba Serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo na vyama vya wafanyakazi   kupata ufumbuzi wa vikokotoo vya mafao ya pensheni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kikao cha kamati ya utendaji, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, alisema vikokotoo hivyo vimepokelewa na wafanyakazi kwa mtizamo hasi lakini wanaamini fursa ya majadiliano itasaidia kuepuka mgogoro kati ya Serikali na wafanyakazi.

Kikao hicho kilikuwa na lengo la kujadili hoja ya kuunganishwa  mifuko ya hifadhi ya jamii na vikokotoo vya mafao ya pensheni kwa wastaafu wa mifuko ya PSSSF na NSSF.

“Kwa kuzingatia hekima na busara na kwa kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi nchini, ni vema Serikali ikaliona hili katika mtizamo chanya kwa kutafuta ufumbuzi utakaoleta tija kwa wafanyakazi na taifa.

“Tunawaomba wafanyakazi wote wawe watulivu, ukweli ni kwamba tangu hatua za awali TUCTA tumeshirikishwa lakini tatizo limekuja kujitokeza kwenye kutungwa kanuni.

“Baada ya kikao hiki tutakutana na waziri, tunaamini amesikia kauli yetu na kilio cha wanachama wetu. Ni imani yetu watalifanyia kazi suala hili kuleta unafuu kwa wanachama wetu,” alisema Nyamhokya.

Shirikisho hilo lilisema awali lilipendekeza mafao ya mkupuo yawe asilimia 40 na asilimia 60 iwe pensheni ya kila mwezi badala ya kanuni za sasa zinazomlipa mstaafu asilimia 25 kama malipo ya mkupuo na asilimia 75 kama pensheni ya kila mwezi.

“TUCTA kama mwakilishi wa wafanyakazi nchini tulishiriki katika mchakato mzima wa kutungwa kwa Sheria ya PSSSF namba 2 ya mwaka 2018 kwa kutoa maoni na msimamo wetu kwenye vikao mbalimbali vya wadau.

“Ni wajibu na haki yetu kusema kwamba mapendekezo yetu kwenye sheria hiyo yalizingatiwa kwa kiwango kikubwa sana tatizo limekuja kujitokeza kwenye kutungwa kanuni,” alisema.

Alisema  katika kutungwa kanuni hizo, Ofisi ya Waziri Mkuu ilishirikisha wadau wote likiwamo shirikisho hilo na kwamba Juni 7 na 8 mwaka huu, walipokea mapendekezo ya vikokotoo hivyo na kuomba muda wa kuvipitia kabla ya kutoa maoni yao.

Alisema Juni 12 kikao kingine kilifanyika Ofisi ya Waziri Mkuu ambako upande wa wafanyakazi kupitia TUCTA waliwasilisha maoni na mapendekezo yao juu ya kanuni zilizopendekezwa na Serikali.

Kwa mujibu wa Rais huyo wa TUCTA, miongoni mwa maoni yao ni Serikali kuendelea na kanuni zinazotoa malipo ya mkupuo (asilimia 50), kikokotoo cha 1/540 na umri wa kuishi baada ya kustaafu miaka 15.5 kwa wafanyakazi waliopo kwenye mifuko.

Hata hivyo, alisema waziri aliwaahidi  tafanyika  tathmini tena kuangalia mali zote za mifuko na uwezekano wa kupandisha kikokotoo.

“Waziri alitupa ushirikiano mkubwa,   tatizo hatukufikia yale tuliyoyataka na Agosti 15 Waziri alituita na kutueleza kuwa majadiliano yanaweza kuendelea hata baada ya kutangazwa   kanuni mpya,” alisema.

Hata hivyo alipoulizwa kwa nini hoja ya kupinga vikokotoo hivyo imekuja sasa wakati Mifuko ya NSSF na PPF walikuwa wakilipa asilimia 25, alisema kuumia kwa mfanyakazi mmoja ni sawa na kuumia kwa wafanyakazi wote.

Kulingana na SSRA vikokotoo vinavyotumika vilianza tangu Julai Mosi, 2014 na tayari wastaafu wa Mifuko ya Pensheni ya NSSF na PPF walikuwa wakipokea pensheni kwa kikokotoo hicho.

Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Dk. Irene Isaka, alikaririwa na vyombo vya habari wiki iliyopita akisema   kilichobadilika ni kiwango cha mkupuo kwa kundi dogo la wanachama takribani asilimia 20 ya wanachama wote wa sekta ya hifadhi ya jamii waliokuwa wakipokea mkupuo wa asilimia 50   wawe sawa na wanachama wenzao wanaopokea asilimia 25.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Je, ni kweli kuwa wastaafu wa serikali wanalazimishwa kupokea pensheni zao kupitia benki ya NMB? Kuna sababu gani kulazimishwa badala ya kuwaruhusu wajichagulie benki waipendayo?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles