VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM
WATOTO tisa kati ya 14 wamefanyiwa upasuaji kutibu magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa njia ya tundu dogo kupitia mshipa mkubwa wa damu kwenye paja.
Upasuaji huo umefanywa na JKCI kwa kushirikiana na mradi wa Little Heart wa Saudi Arabia ambao ni moja ya miradi ya afya ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao yake makuu London, Uingereza.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto JKCI, Naiz Majani alisema watoto watano wamefanyiwa upasuaji kwa njia ya kufungua kifua.
Alisema kambi hiyo ya matibabu ilianza rasmi Ijumaa iliyopita na wamekusudia hadi itakapokamilika watakuwa wametibu wagonjwa 80.
“Matatizo ya moyo ya utotoni hupaswa kugundulika na kutibiwa utotoni, wengi hufariki dunia ingawa wapo watu wazima pia ambao hubahatika kuishi muda mrefu, tunakusudia kuwatibu,” alisema.
Dk. Naiz alisema hiyo ni awamu ya tano tangu mwaka 2015 hadi sasa kushirikiana na taasisi hiyo na kwamba ndilo kundi pekee ambalo hutibia idadi kubwa ya wagonjwa.
“Kwa mwaka huu malengo yetu tuliyokuwa tumejiwekea tumeweza kuyafikia kwa kiwango cha asilimia 80, yaani tulikusudia kuwafanyia matibabu wagonjwa 400 tumeweza kuwafikia 300 tu.
“Hali hiyo imesababishwa na changamoto ya ufinyu wa nafasi, ambayo inashughulikiwa hivi sasa… tunatarajia mwakani ukarabati wa jengo utakuwa umekamilika,” alisema.