24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Rushwa ya ngono UDSM lachukua sura mpya

Na Evans Magege-DAR ES SALAAM



SAKATA la tuhuma za ngono dhidi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), limechukua sura mpya huku Serikali ikitangaza kuingilia kati ili kupata ukweli wa suala hilo.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuibuliwa kwa tuhuma hizo na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Vicensia Shule, kupitia akaunti yake ya mtandao wa Twitter, zimeonekana kutikisa taasisi hiyo ambapo jana kamati yake ya nidhamu ilikutana kuanza kuchunguza kashfa hiyo.

Katika akaunti yake ya twitter Dk. Shule juzi alindika;  “Baba MagufuliJP (Rais John Magufuli) umeingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufungua maktaba ya kisasa. Rushwa ya ngono imekithiri mno UDSM.

“Nilitamani nikupokee kwa bango langu ila ulinzi wako umenifanya ninyamae. Nasubiri kusikia toka kwako maana naamini wateule wako ni waadilifu watakwambia ukweli”.

Akizungumza na MTANZANIA jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, alisema wizara imelisikia suala hilo kupitia vyombo vya habari na hatua ya awali watawasiliana na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ili kupata maelezo yao kuhusu suala hilo.

“Ninachoweza kusema kwa sasa hatua za awali ambazo tutachukua ni kuwasiliana na uongozi wa chuo kikuu (UDSM) ili kupata maelezo yao kuhusu suala hilo. Maana suala la tuhuma za ngono si dogo kwa taasisi kubwa ya elimu.

“Pia tutaunga kamati ya uchunguzi ili kuweza kujua ukweli wa suala hili na wale ambao watabainika basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. kwa sasa ninaweza kukueleza hivyo,” alisema Dk. Akwilapo.

KAULI YA TAHLISO

Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilimtafuta Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania ( TAHLISO), George Mnali, ambapo alisema suala hilo lipo katikati kwa maana kwamba linafahamika au kutofahamika kwani ni jambo linalofanywa kwa usiri mkubwa.

Alisema hali hiyo inatokana na wahusika wa kutoa rushwa za ngono huwa wamekubaliana na mazingira.

Alitolea mfano matukio kama hayo yaliwahi kutokea katika chuo kimoja mkoani Iringa (jina limehifadhiwa),  kwamba kuna mwanafunzi alipewa ‘disco’ (kafelishwa) kwa kisa cha rafiki yake wa kike (mpenzi) kumkataa kingono mkuu wa Idara ya Sheria ambayo yeye na rafiki yake walikuwa wanasoma.

“Jamaa ilifikia hatua akapata disco akiwa mwaka wa tatu. Yaani alikuwa mwaka wa tatu muhula wa mwisho na huyo rafiki (mpenzi) wake akapewa supp ya somo moja pia akacheleweshwa kupokewa kwa research yake,” alisema.

Alikwenda mbali kwa kusema kwamba rushwa ya ngono ni kitu ambacho kipo katika mazingira ya vyuo vikuu lakini wanafunzi hasa waathiriwa wapo kwenye wakati mgumu wa kuliweka wazi suala hilo.

“ Wanafunzi wanashindwa kuweka wazi jambo hili kwa sababu wakati nyumbani wanataka shahada, chuoni  mwalimu naye kaishikilia shahada yake mpaka apate timizo la ngono, kwa hiyo unakuta kunavitu vinakuwa kwenye ubinafsi mkubwa na hata ukiwauliza wanaweza wasikwambie japo wanaumia.

“Lakini nimeongea na marais kutoka vyuo vitatu wanasema kwamba imefikia wakati wao wanajitoa mhanga kwamba mwanafunzi akienda kuripoti kwao inabidi rais amwagize binti huyo akamwambie mwalimu kuwa yeye ni rafiki wa kimapenzi wa rais wa chuo.

“Inabidi rais watumie mbinu hiyo ili kumlinda mwanafunzi kwa sababu walimu wanaofanya uchafu huo huwa na kawaida ya kuwaogopa marais wa vyuo lakini bado kuna rais mmoja alifanya hivyo naye akajikuta analimwa suup na huyo mwalimu.

“Baada ya rais kufuatilia sana jambo hilo mwalimu akamwambia haikuwa supp bali hakuiona karatasi yake ya mitihani wakati anasahihisha.

“ Rais alipofuatilia kwenye bodi ya mitihani akaambiwa karatasi yake ilikuwapo na aliporejea kwa mwalimu muhusika, mwalimu huyo akaomba msamaha kwa kumtaka asiende kuripoti kwa mkuu wa chuo,” alisema.

Alisema suala la rushwa ya ngono si tu linawaumiza mwanafunzi wa kike bali hata wa kiume hasa wale wenye urafiki wa kimapenzi na mabinti wanaohitajiwa kimapenzi na walimu.

Alisema kuwa pamoja na kwamba kesi za rushwa ya ngono haziwasilishwi kwa njia ya maandishi lakini suala hilo linazungumzwa na marais wa vyuo.

Alisema yeye kama raisanapendelea kuwapo mfumo wa waathiriwa kupaza sauti ya malalamiko yao.

Alisema kwa mazingira yalivyo sasa vyuoni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa (Takukuru) inatakiwa kutengeneza dawati  maalumu la kupambana na rushwa za ngono kwa wanafunzi.

WANAFUNZI KUWATEGA WALIMU

Katika hatua nyingine Mnali alisema suala la rushwa ya ngono si tu kwa walimu kuwataka wanafunzi bali hata baadhi ya wanafunzi wamekuwa na tabia ya kuwataka walimu.

Alisema kuwa wanafunzi wamekuwa wakijenga mazingira ya urafiki wa kimapenzi na walimu ili wapate msaada wa alama za ufaulu kwenye baadhi ya masomo

“ Wakati mwingine sio kwamba walimu wanalazimisha ila ni baadhi ya wanafunzi wanawalazimisha walimu , unakuna mwanafunzi anaona somo ni gumu hivyo anaamua kumtega mwalimu  kimapenzi  kwa lengo la kuepuka kufeli somo

“ Kwa hiyo hili suala la rushwa ya ngono ni suala la kuviziana pande zote, nasema hivyo kwa sababu mwanafunzi wa kike akiona kabanwa sana  na mwalimu alafu somo haliwezi, hata kama mwalimu hana mpango naye nawaweza kutumia mbinu ya kumtega kimapenzi ili kumnasa mwalimu ampe alama za ufaulu,” alisema Mnali.

RAIS TURDACO

Katika hatua nyingine gazeti hili lilizungumza na Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumain Kampasi ya Dar es Salaam(TURDACO), Benjamin Mayala ambaye alisema kwa upande wa chuo chao hakujawahi kuripotiwa tukio lolote la rushwa ya ngono lakini anaamini kuwa matukio hayo yapo katika ngazi za vyuo vikuu.

Alisema Serikali ya Wanafunzi wa TURDACO ina mfumo maalumu ambao unampa nafasi mwanafunzi kuripoti malalamiko yake lakini tangu aingie madarakani Juni mwaka huu, hakuna kesi yoyote inayohusiana na rushwa ya ngono iliyoripotiwa.

Alisema kwa kutambua uwapo wa tatizo la rushwa ya ngono katika ngazi ya vyuo vikuu, uongozi wa serikali yake wiki iliyopita ilikutana na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), katika Chuo cha Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kuzungumzia tatizo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles