Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Rais Dk John Magufuli amemtuma Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowasa kuwafikishia ujumbe viongozi wenzake wa upinzani watulie na kutii sheria za nchi la sivyo wataishia magerezani.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 27, walipokutana na Lowasa katika ufunguzi wa maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Rais Magufuli pia amemshukuru na kumsifu Lowasa kwa kuwa mtulivu siku zote hata baada ya kumshinda katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.
“Mzee Lowasa wewe ni kiongozi wa kuigwa, nilipokugalagaza kwenye uchaguzi ukaenda kutulia zako pembeni, wanaopiga kelele wala hawakaugombea , wewe ni mfano bora kwakweli hongera kwa hilo.
“Nimeongea hili kwa heshima ili mzee Lowasa wale unawaongoza ukawashauri la sivyo wataishia magerezani ili wakajifunze kutii sheria za Tanzania, “ amesema.
Aidha Magufuli amesema utofauti wa vyama siasa isiwe chanzo cha kuwatenganisha watanzania bali iwe chachu ya kuleta maendeleo katika taifa.