26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Umoja wa Ulaya waidhinisha makubaliano ya Brexit

BRUSSELS, UBELGIJI



VIONGOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) wameunga mkono makubaliano ya Uingereza kuondoka katika Umoja huo pamoja na mkataba wa uhusiano wa siku za mbele kati ya pande hizo mbili.

“Viongozi wa mataifa 27 yaliyobakia Umoja wa Ulaya wameunga mkono makubaliano na azimio la kisiasa kuhusu uhusiano wa baadaye kati ya umoja huo na Uingereza”, ameandika Mwenyekiti wa Baraza la Ulaya, Donanld Tusk katika ukurasa wake wa Twitter, akigusia nyaraka mbili zilizotiwa saini jana mjini hapa.

Nyaraka hizo zinahalalisha kujitoa rasmi kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya Machi 19, 2019 pamoja na kufungua njia ya kuanza mazungumzo kuhusu mustakabali wa uhusiano wa siku za mbele kuanzia kisiasa hadi kibiashara.

Hata hivyo kwa sasa, Waziri Mkuu wa UIngereza, Theresa May anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kuwashawishi wabunge wa Taifa hilo waunge mkono makubaliano yaliyofikiwa.

Mkataba wa Brexit umezusha lawama kali kutoka kwa wale wanaoupinga Umoja wa Ulaya kama ilivyo kwa wale wanaouunga mkono nchini Uingereza.

Mwenendo huo unatia wasiwasi iwapo utaweza kuungwa mkono utakapofikishwa bungeni kupigiwa kura katikati ya Desemba mwaka huu.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamewatolea wito wabunge wa Uingereza waunge mkono makubaliano yaliyofikiwa.

“Kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ni tukio la majonzi makubwa,” alisema Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker.

Hata hivyo, ameeleza matumaini yake kuwa Bunge la Uingereza litaunga mkono mkataba huo wa Brexit.

Akiulizwa ushauri wake kwa wabunge wa Uingereza, Juncker alisema angekuwa yeye angepiga kura kuunga mkono kwasababu  huo ni mkataba bora zaidi kwa Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte pia amewatolea wito wabunge wa Uingereza waunge mkono makubaliano hayo.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kwa upande wake makubaliano ya Brexit yanabainisha udhaifu wa Umoja wa Ulaya na kuwataka viongozi wenzake waunge mkono mageuzi ya kina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles