27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

AG avunja ukimya jalada la vigogo mwendokasi

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM



MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Adelardus Kilangi, kwa mara ya kwanza amethibitisha kupokea jalada wafanyakazi wanane wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka ya Uda-Rapid Transit (UDART), akiwamo kigogo wa Idara ya Fedha wa kampuni hiyo huku akisema kuwa pindi atakapokamilisha taratibu za kisheria watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.

Wafanyakazi hao ambao kwa sasa bado wanaendelea kusota mahabusu kwa zaidi ya siku 60, wanadaiwa kuhusika na mtandao wa kufyatua tiketi feki na kujipatia mamilioni ya fedha huku serikali kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART ) ikikosa mapato.

Hatua hiyo ililifanya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kulifananisha kosa hilo na uhujumu uchumi.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, AG, Dk. Kilangi alisema jalada la wafanyakazi hao lipo ofisini kwake ili waweze kuchukua hatua zaidi za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipitia na pindi atakapokamilisha watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.

“Siwezi kuzungumzia suala hili kwa undani zaidi kwa sababu bado linafanyiwa kazi ikiwa tutakamilisha, tutawapeleka mahakamani,” alisema Dk. Kilangi.

Hata hivyo, mwishoni mwa wiki Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar as Salaam, Lazaro Mambosasa alipozungumza na gazeti hili alisema bado wanaendelea kuwashikilia vigogo hao kwa ajili ya uchunguzi zaidi huku akidai jalada lao tayari limepelekwa kwa AG kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

“Jeshi la Polisi linaendelea kuwashikilia wafanyakazi hao kwa hatua zaidi za uchunguzi baada ya kukamilika na AG kutoa uamuzi wake, tutawafikisha mahakamani,” alisema Mambosasa.

Inadaiwa kuwa, kigogo huyo alikuwa akiongoza timu ya wafanyakazi ambao pia walikuwa wakiuza tiketi za mabasi za wanafunzi za Sh 200 kwa watu wazima huku zile za watu wazima za Sh 650 zikiuzwa mara mbili na hata nyingine zikiwa hazitambuliki kwenye mfumo.

Kukamatwa kwa wafanyakazi hao zaidi ya 30 kulitokana na taarifa zilizoibuliwa na MTANZANIA katika ripoti maalumu Juni mwaka huu ambayo pamoja na mambo mengine, ilieleza hujuma mbalimbali  zinazofanywa na wajanja wachache huku serikali ikikosa mapato.

Septemba 24, mwaka huu wafanyakazi zaidi ya 50 UDART, wa vituo vya Kimara na Gerezani   Dar es Salaam, walikamatwa na polisi kwa tuhuma za kutoa tiketi feki kwa abiria wanaoutumia mabasi hayo.

Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa kwa   miezi miwili ilibanika kushuka kwa kasi kwa mapato ya Kituo cha Kimara kutoka makusanyo ya Sh milioni 20 hadi Sh milioni 25 kwa siku wakati yaliyokuwa yakikisanywa kupitia mfumo wa eletroniki na kufikia hadi Sh milioni 10 kwa siku.

Hatua hiyo iliifanya Serikali kupitia Wakala wa  Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) kufanya uchunguzi wa kina na kubaini mtandao huo wa wizi huku mmoja wa kigogo wa juu wa Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART), naye akishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kuhusishwa na mtandao huo.

Wafanyakazi hao baada ya kuchujwa 18 walibainika kuhusika moja kwa moja na mtandao huo kwa kilichoelezwa kuendesha vitendo vya uhujumu uchumi katika mradi huo wa serikali.

Inadaiwa wafanyakazi hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wengine wanadaiwa kuunda mtandao maalumu wa kufyatua tiketi feki na kujipatia mamilioni ya fedha.

Mradi huo wakati unaanza mwaka 2016, ulikuwa unabeba abiria 75,000 na kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 200,000.

Katika mtandao huo imebainika mbali ya kufyatua tiketi feki pia wamekuwa wakifanya ujanja kwa kuwauzia watu wazima tiketi za wanafunzi za Sh 200 badala ya Sh 650 huku kiwango kinachobaki kikingia katika mifuko ya wajanja.

Aprili 24 na Mei 16, mwaka huu makusanyo yalianza kuhujumiwa baada ya UDART kuingilia kati na kutaka kukusanya wao fedha huku wakipinga  tiketi za elektroniki za Kampuni ya Maxcom Afrika Plc.

Hatua hiyo iliifanya UDART kuingilia na kusimamia ukusanyaji wa mapato kupitia tiketi maalumu za mashine ambazozilikuwa zikichanwa na wafanyakazi waliowekwa milango.

Mradi huo ulipoanza, suala la makusanyo lilikuwa chini ya Kampuni ya Maxcom Africa ambao walikuwa wakikusanya kwa mfumo wa elektroniki na udhibiti wa wizi huku UDART wakibaki na uendeshaji mabasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles