MTANZANIA mzaliwa wa Mkoa wa Iringa, Julio Ludago, anatarajia kuvunja rekodi ya dunia ya kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro kwa kutumia muda mfupi zaidi bila kuwa na usaidizi wowote.
Mtanzania huyo anayefanya kazi katika kampuni ya kutembeza watalii ya Ahsante Tours, anataka kuvunja rekodi mbili kubwa zaidi zilizowekwa na Mswisi na Mtanzania, siku ya Septemba 27 mwaka huu, atakapopanda mlima huo.
Ecuadorian Karl Egloff kutoka Uswisi ndiye anayeshikilia rekodi ya kupanda na kushuka mlima huo, huku akiwa na usaidizi alipotumia saa 6.45 mwaka 2014.
Rekodi nyingine inashikiliwa na Mtanzania, Saimon Mtui, aliyepanda na kushika mlima huo kwa kutumia saa 9.19 bila kuwa na usaidizi wowote.
“Najua kuvunja rekodi ya dunia si kitu rahisi, kuna changamoto nyingi za hatari katika mlima huo, lakini nimejipanga kuvunja rekodi hiyo kwa kuwa nimefanya mazoezi kwa miezi miwili kwa msaada kutoka kampuni ya Intel, Ahsante Tours na ASUS I, hivyo nimejiandaa vya kutosha kuvunja rekodi hiyo siku hiyo ya Septemba 27,” alisema Julio.