Nora Damian, Tunduru
Diwani wa Kata ya Nalasi Magharibi, Khalifa Kabango (CUF), anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Tunduru kwa tuhuma za kulangua korosho kwa wakulima kwa bei ya Sh 1,500 kwa kilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Novemba 19, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homela, amesema diwani huyo alikamatwa juzi kutokana na operesheni iliyofanywa katika Tarafa ya Nalasi.
Amesema katika tarafa hiyo vilikamatwa viroba 31 vikiwamo vya diwani huyo.
“Huyu diwani alikutwa ananunua korosho kutoka kwa wakulima kwa bei ya Sh 1,500 ili apeleke vyama vya msingi akapate fedha zaidi,” amesema Homela.
Amesema pia katika operesheni iliyoanza Oktoba hadi sasa wamekamata tani 23 za korosho zenye thamani ya Sh milioni 75.
Kwa mujibu wa DC huyo baadhi ya matajiri wamekuwa wakituma fedha vijijini na wenyeji ndiyo wanaonunua korosho hizo.
“Wenyeji ndiyo wanaonunua baada ya kutumiwa fedha na matajiri halafu wakikamatwa wanawataja mabosi waliowatumia,” amesema.