Na MWANDISHI WETU-MOROGORO
MSIMAMO wa kulinda na kutetea masilahi ya taifa unaofanywa na Rais Dk. John Magufuli, umewasha moto ndani ya CCM Mkoa wa Morogoro huku viongozi wa chama hicho wakiweka wazi msimamo dhidi ya watu wanaothubutu kumkwamisha.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mjini hapa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Innocent Kalogelesi alisema hotuba iliyotolewa na Rais Magufuli hivi karibuni wakati akiwaapisha mawaziri wapya Ikulu Dar es Salaam, inahitaji kuzingatiwa kwa makini na kufanyiwa kazi na watendaji wenye dhamana kwa umma hasa wa wizara, idara na halmashauri nchini.
Alisema hatua ya serikali kununua korosho kwa bei ya Sh 3300 kwa kilo moja na kutowalamba miguu au kuwabembeleza wafanyabishara wanyonyaji, inakwenda kuleta matokeo halisi kwa taifa ikiwamo CCM Mkoa wa Morogoro.
“Kuwazuia wanunuzi wababaishaji ambao kwa makusudi wamechelewa kupeleka taarifa za ununuzi wa korosho na kuambiwa wasisumbuke ni ujasiri. Kumethibitisha msimamo wa serikali katika kutetea tija na masilahi ya wakulima,” alisema Kalogeles
Alisema CCM Mkoa wa Morogoro inaamini mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, hayakufanyika kwa nia mbaya bali yameongeza motisha na kusukuma mbele gurudumu kwa kutoa manufaa kwa wakulima nchini wakiwamo wa korosho kwa kuwa na uhakika na mazao yao kupata soko la uhakika.
“Mawaziri na watendaji wengine waliopewa dhamana maeneo ya utawala, wanapaswa kutambua mahali tulipo sasa.
“Hapa tulipo tumechelewa mno. Tumejikwamisha kutokana na utapeli, ubabaishaji , urasimu au kuendekeza mawazo mgando,” alisema
Alisema Rais Dk. Magufuli amekuwa mstari wa mbele kupigania mageuzi ya maendeleo akitaka nchi ijenge uchumi imara wa kujitegemea.
“Ni wazi Watanzania wenzangu sasa nchi yetu imepata jemedari ambaye ameifanya iwe na heshima kwa kuwa na uchumi imara na ni wazi tunakwenda kuondokana na utegemezi wa kuwa ombaomba.
“Tunazo rasilimali sasa ni wajibu wetu kusimamia kwa masilahi ya Watanzania wote.
“Tukatae kusikiliza hadithi za matapeli wanaotumiwa na mabeberu au makabaila wenye lengo la kuwnyonya wananchi.
“Wapo wanaotaka kujitajirisha ili wanufaike kwa jasho la wengine. Tukikubali utumwa huo wa fikra kundi kubwa la wananchi litakosa huduma muhimu za jamii,” alisema Kalogeles.
Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, alitoa wito kwa kuwataka watendaji wa Serikali ngazi za vijiji, kata, tarafa, wilaya za Mkoa wa Morogoro , wazinduke na kutambua wajibu wao kwa kufanyakazi kwa masilahi ya wananchi kama anavyoagiza Rais Dk. John Magufuli.