Na Janeth Mushi-Longido
WAZIRI Ofisi ya Rais – Tamisemi, Suleiman Jafo, amezitaka wilaya zote nchini zisizokuwa na hospitali za wilaya zianze ujenzi mara moja ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Aidha amewaagiza wahandisi katika maeneo hayo waache tabia ya kukaa ofisini na badala yake wasimamia miradi hiyo kikamilifu.
Jafo amesema hayo Novemba 15 wilayani hapa Mkoa wa Arusha, alipotembelea na kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Longido na Kituo cha afya cha Eworendeke.
Amesema Serikali imetoa Sh. Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Longido ambayo hadi kukamilika kwake itagharimu zaidi ya Sh. Bilioni 1.5.
Ameagiza ujenzi wa hospitali ya wilaya hapa Longido uanze kwa kufuata mchoro wa ramani uliotolewa na Tamisemi ili ramani zote za wilaya zifanane.
“Katika wilaya nyingine ambazo fedha zimeshatengwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya, ujenzi uanze ili ifikapo Novemba 30, mwaka huu baadhi ya huduma ziweze kuanza ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi,”
Waziri Jafo amesema anafurahishwa na ujenzi na uboreshaji wa hospitali pamoja na vituo vya afya unaendelea katika wilaya mbalimbali za mkoani Arusha.
“Nafurahishwa na ujenzi pamoja na uboreshaji wa huduma za afya Mkoa wa Arusha ila nasisitiza wahandisi kusimamia ujenzi wa miradi hii kwa umakini kwani baadhi yenu mnakaa ofisini muda mwingi badala ya kusimamia ujenzi,” ameongeza.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Kimokouwa, kinapojengwa kituo hicho cha afya, Victor Kabati amesema kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi hao ambap wamekuwa wakifuata huduma za afya mbali na wanapoishi.
“Wananchi wengi wanapata shida ya kupata huduma za afya na kuwalazimu kwenda hadi nchi ya jirani hapa mpakani (Kenya), lakini ujenzi wa kituo hiki utasaidia kuondoa usumbufu wa kufuata huduma za afya umbali mrefu,” amesema.