NA CHRISTOPHER MSEKENA
BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), limekuwa likifanya kazi nzuri ya kuchunga mwenendo wa sanaa kwa masilahi makubwa ya mashabiki ambao huitumia sekta hiyo katika maisha yao ya kila siku.
Katika kipindi hiki ambacho kuna kizazi kipya kwenye muziki wa Bongo Fleva, changamoto imekuwa ni namna ambavyo Basata kama walezi wa sanaa wanaweka mipango kuhakikisha wasanii wanatoa muziki mzuri.
Mfano wiki hii wimbo Mwanza ambao umeimbwa na Rayvanny na Diamond Platnumz, wameufungia kutochezwa au kutumbuizwa popote pale nchini Tanzania kutokana na kuwa na lugha chafu zinazohamasisha ngono.
Nimekuwa nikisikiliza nyimbo za wasanii wetu wa Bongo Fleva kwa muda mrefu sasa sababu ni muziki ninaopenda kama unavyopendwa na vijana wengine katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Jambo ambalo nimejifunza ni kukosekana kwa ubunifu unaopelekea wasanii kutumia tungo nyepesi nyepesi ambazo wakati mwingine zinashindwa kuficha matusi na hamasa za ngono zilizopo ndani yake.
Nyimbo za sasa hivi hazina ubunifu, wasanii hawaumizi kichwa kiasi cha kushindwa kuunda mafumbo ambayo hayataleta picha ya moja kwa moja kama ambavyo wanamuziki wa zamani walifanya.
Wanamuziki zamani walifanikiwa kutunga nyimbo zenye mafumbo na muda mwingine zina matusi ndani yake, lakini mpaka mtu ajue kama kuna tusi lakini achekeche kichwa kweli kweli.
Si kwamba zamani wanamuziki walikuwa hawatumii tungo tata kwenye nyimbo zao. Vipo vibao vingi ambavyo ndani yake kulikuwa na mafumbo yaliyojaa lugha za faragha kiasi ni watu wazima tena werevu pekee waliweza kufahamu.
Licha ya sanaa kutakiwa kuwa na uwanda mpana, lakini ukweli ni kwamba kiwango cha kufikiria tungo zenye mafumbo kimepungua mno miongoni mwa wasanii wa leo kiasi inawaudhi watu waungwana ambao wanashindwa kusikiliza muziki wakiwa na watu wanaowaheshimu.
Hali kadhalika Basata wanapaswa kuongeza makali ya kanuni zao hasa ile ya msanii kuwasilisha barazani kazi zake kabla haijatoka kwenye jamii ili kuepusha hiki ambacho kimetokea punde baada ya Rayvanny na Diamond Platnumz kuachia wimbo wao.
Ni kitendo cha mara moja cha Basata, kuwasiliana na wamiliki wa vyombo vya habari na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuacha kucheza nyimbo ambazo hazina muhuri wao ili kudhibiti hali ya kufungia nyimbo wakati tayari zipo mtaani.
NUKUU
“Ifike kipindi kama unahitaji kufanya kitu kikubwa basi hakikisha ‘role model’ wako ni wewe mwenyewe, fanya kitu unachokiona wewe tu,”
Creator Pro Films.