Veronica Romwald, Dar es Salaam
Wataalamu wa watoto wachanga kutoa mikoa mbalimbali nchini kwa mara ya kwanza wamekutana Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kujadili na kupeana mbinu zitakazosaidia kukabiliana na vifo vya watoto hao.
Akifungua kongamano hilo, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, amesema Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la vifo vya watoto wachanga chini ya mwezi mmoja.
“Asilimia kubwa ya vifo hivyo huwa ni watoto waliozaliwa kabla ya kutimiza umri wa miezi sita (njiti), takwimu zinaonesha kati ya asilimia 13 hadi 17 ya watoto wanaozaliwa nchini, huzaliwa wakiwa njiti.
“Serikali kupitia Wizara imekuwa ikiratibu programu mbalimbali kupunguza idadi ya vifo vya watoto hawa, lakini pia kwa kushirikiana na Tamisemi tumehakikisha kila hospitali nchini ina wodi ya kuhudumia watoto wachanga,” amesema.
Akizungumza, Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Watoto Tanzania (PAT), Dk. Sekela Mwakyusa amesema hali hiyo ndiyo iliyowasukuma kufanya kongamano hilo ili kuja pamoja kujadiliana na kupeana mbinu mbadala.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Watoto Wachanga Muhimbili, Edna Majaliwa amesema kauli mbiu ya Kongamano la Kwanza la Kisayansi la Wataalamu wanaohudumia Watoto Wachanga katika hospitali zote za rufaa nchini inasema ‘Kila Pumzi ina Thamani’.
Amesema kwa kawaida katika kitengo hicho hupokea watoto kati ya 70 hadi 90 lakini kuanzia kipindi cha Oktoba hadi Mei hupokea idadi kubwa zaidi kati ya watoto 200 hadi 250.