Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema Rais Dk. John Magufuli amekubali kukutana na kuzungumza na viongozi wa vyama vya siasa na wa dini kuhusu mustakabali wa taifa.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), alitoa kauli hiyo juzi muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Dar es Salaam.
“Tumezungumza na Rais Magufuli mambo ya msingi kuhusu taifa letu, tulikuwa tumeomba tangu mwaka jana na mwaka juzi sisi ndani ya TCD kwa kuwa Tanzania ni yetu wote… mama Tanzania akipata upendo basi Tanzania yote itakuwa imepata manufaa kwenye kuzingatia nguzo tatu katika wimbo wetu wa taifa, yaani hekima, umoja na amani.
“Kwahiyo Rais katupokea vizuri na kasema yuko tayari tuzungumze na vyama vya siasa vyote na viongozi wa dini kwa sababu ni taasisi ambazo ni sehemu ya Tanzania.
“Kwahiyo tukiwa na meza ya mazungumzo, majadiliano ya kitaifa mambo yatakwenda vizuri.
“Tulizungumza pia masuala ya elimu, afya na tumezungumza Tanzania tunayotaka iwe ya aina gani na tumekubaliana mahali popote panatokea mambo hayako sawa kwa taifa, basi tutumie hekima, umoja na amani. Mahali penye umoja maendeleo endelevu yanapatikana kwa masilahi ya mama Tanzania.
“Pia nimezungumza naye mambo ya jimboni kwangu Vunjo na nimemkaribisha, lakini amesema pamoja na kazi nyingine za maendeleo tunazozifanya, anaunga mkono kwa masilahi endelevu kwa ajili ya wananchi wote,” alisema Mbatia.