MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeacha kwa muda kusikiliza kesi ya kughushi hati ya umiliki wa nyumba inayomkabili mfanyabiashara Marijan Abubakar, maarufu kama Papaa Msofe (50).
Mahakama hiyo iligoma kuifuta kesi hiyo jana katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mkazi, Renatus Rutta baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na pande mbili zinazopingana.
Wakili wa utetezi, Majura Magafu aliwasilisha hoja katika mahakama hiyo akidai kwamba mteja wake anakabiliwa na kesi nyingine katika Mahakama ya Ardhi na nyaraka zilizowasilishwa huko ndizo zilizowasilishwa katika Mahakama ya Kisutu.
Magafu aliomba kutokana na sababu hizo za kufanana kwa nyaraka aliomba kesi hiyo isitishwe kwa muda kusikilizwa hadi ile iliyopo Mahakama ya Ardhi itakapomalizika.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Wankyo Simon, ulipinga maombi hayo na kuiomba mahakama kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Ruta alisema mahakama haiwezi kusimamisha usikilizaji wa kesi hiyo kwa sababu ndio yenye mamlaka ya kutoa uamuzi wa kesi za kughushi.
Hakimu Ruta baada ya kuamua hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 2 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Msofe kwa mara ya kwanza alifikishwa kortini Agosti 2012 akikabiliwa na kesi ya mauaji pamoja na mwenzake ambapo Juni mwaka huu waliachiwa huru na kesi hiyo kufutwa.
Msofe alifunguliwa kesi mpya ambapo anadaiwa kuwa Desemba 23, 2004 katika Wilaya ya Ilala alighushi nyaraka ya kuhamisha haki ya umiliki wa nyumba namba 288 ambayo ni mali ya mfanyabiashara wa madini marehemu Onesphory Kituli.
Ilidaiwa kuwa Msofe kwa nia ya kudanganya alighushi nyaraka hiyo akionyesha Desemba 13, 2004 Kituli alihamisha haki yake ya umiliki wa nyumba hiyo kwake wakati akijua ni uongo.
Mbali na shtaka hilo, Msofe anadaiwa kuwa kati ya Desemba 23, 2004 na Machi 30, 2005 akiwa na nia ya kudanganya alitoa nyaraka hizo za uongo kwa Kamishna wa Ardhi kwa lengo la kuhamisha umiliki kutoka kwa Kituli kwenda kwake.