26.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

CCM yajitabiria ushindi asilimia 69.3

Pg 3NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema takwimu zinaonyesha mikutano yote iliyofanywa na mgombea urais wake, Dk. John Magufuli hadi sasa, kinaweza kuibuka na ushindi wa asilimia 69.3.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya chama hicho, January Makamba, alisema takwimu hizo zimetokana na utafiti wa ndani uliofanywa siku kumi zilizopita katika majimbo 246 kati ya 269.

“Utafiti huu ulishirikisha taasisi nyingine binafsi, unaonyesha Dk. Magufuli atapata ushindi wa asilimia 69.3. Tunatarajia ushindi huu utaongezeka kadiri Watanzania wengi wanavyozidi kumsikiliza mgombea, ilani na sera zake,” alisema Makamba.

Alisema takwimu hizo, zinajumuisha mkutano wa juzi mkoani Tabora na kukamilisha mikoa 12 na majimbo 94, ambapo alisikilizwa na wapigakura asilimia 70.

Kwa upande wa ubunge, Makamba alisema zaidi ya robo tatu ya wagombea wa chama hicho, wamekwishazindua kampeni zao.

Alisema sekretarieti ya kampeni inaandaa mpango  maalumu kwenye majimbo ambayo yanakabiliwa na upinzani.

“Nawajulisha wana CCM, viongozi, makada waliopo madarakani na wastaafu watapita majimbo yote nchi nzima siku 30 za mwisho kwa nia ya kuongeza ushindi wa CCM na mgombea wake,” alisema.

 

MDAHALO

Kuhusu mdahalo, Makamba alisema wiki tatu zilizopita walipokea mwaliko wa kuomba Dk. Magufuli ashiriki mdahalo wa urais utakaoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Twaweza.

Alisema kwa kuzingatia umuhimu wa mdahalo huo utakaoshirikisha pia vyama vingine, CCM imekubali ombi hilo.

“Kwa msingi huo, kauli ya Ukawa iliyotolewa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia kwamba inaomba mdahalo ni kuwahadaa Watanzania… mwaliko ulitolewa mapema kwa vyama vyote na wanaotakiwa kushiriki ni wagombea urais wa vyama.

“CCM inafurahishwa na utamaduni wa midahalo ambao unaanza kujitokeza katika chaguzi zetu, kwa sababu ni sehmu muhimu ya kushirikisha wapigakura katika mchakato wa uchaguzi mkuu utakaowasaidia wamchague nani kwa misingi ya hoja, sera na sio kwa ushabiki, propaganda na mihemiko,” alisema.

Alisema midahalo hutoa nafasi kwa wagombea kuulizwa maswali ya moja kwa moja na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu sera, ahadi zao, fursa ambayo hawaipati kwenye mikutano ya hadhara ya kampeni.

Aidha Makamba alitoa wito kwa vyama vinavyoshiriki uchaguzi wa mwaka huu, kushiriki kwa amani na kuacha kutoa kauli zinazohatarisha amani ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles