Na Othman Miraji
KUTOKANA na kitendo cha uongozi wa Ufalme wa Saudi Arabia kumuua mwezi uliopita Mwandishi wa Habari Jamal Khashoggi, vita vya Yemen sasa vinashuhudiwa waziwazi na walimwengu.
Vita hivyo vilianza Machi 2015 pale mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, alipoyatuma majeshi ya nchi yake yaivamie Yemen, yakisaidiwa pia na majeshi ya nchi nyingine kama vile Umoja wa Falme za Kiarabu. Matokeo ya uvamizi huo yameelezewa na Umoja wa Mataifa ni sababu ya kuzuka janga na maafa makubwa kabisa kushuhudiwa hivi sasa. Marekani na Uingereza haziwezi kuepuka kulaumiwa juu ya sababu ya maafa hayo. Bila ya nchi hizo kuiuzia Riyadh silaha, Ufalme huo katu usingeweza hadi sasa kuendelea na vita hivyo.
Afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeowanisha utoaji wa misaada huko Sanaa, Lise Grand, ametoa tahadhari ya haraka akionya kwamba ikiwa vitendo vya Saudi Arabia vya kuzizingira bandari za Yemen na kuishambulia nchi hiyo kwa mabomu kutoka angani havitakoma, basi nchi hiyo itajionea balaa kubwa la njaa ambalo halijawahi kushuhudiwa mnamo miaka 100 iliyopita. Aliendelea kusema kwamba watu wengi hawajawaza kwamba hali kama hii ingeweza kutokea.
Naye Mark Lowcock, mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeowanisha shughuli za misaada ya dharura, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, alipokuwa anaielezea sura ya kusikitisha ya hali ya mambo, kwamba katika Vita vya Yemen hadi sasa watu 28,000 wamekufa, wengi wao wakiwa ni watoto, miundombinu mingi imeharibiwa, nusu ya hospitali zilizokuwapo zimeteketezwa na zilizobaki zimejaa wagonjwa pomoni.
Kuna malaki kwa malaki ya wakimbizi wa ndani. Pia tangu mwanzo wa mwaka huu sarafu ya Yemen- Riyal-imeshuka thamani yake kwa nusu na vyakula vimezidi kuadimika.
Asilimia 80 ya Wayemeni wanaishi katika umaskini ambapo kabla ya vita idadi yao ilikuwa asilimia 38. Kweli, Yemen maisha imekuwa nchi iliyo maskini kabisa katika Bara Arabu, lakini tangu vita vianze mwaka 2014 mambo yamezidi kuwa mabaya.
Vita hivi vinatokana na hali ya ovyo iliyopo katika nchi hiyo na pia wakati huo huo vimechochewa na ushindani baina ya Saudi Arabia na Iran. Nchi hizo mbili zina wawakilishi wao katika vita hivyo. Serikali ya nchi hiyo inayotambuliwa kimataifa na inayoongozwa na Rais aliye uhamishoni Riyadh, Abdrabbuh Mansour Hadi, inaungwa mkono na majeshi ya Nchi za Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.
Wahouthi ( asilimia 30Â ya wakaazi wa Yemen), walio wa madhehebu ya Zaydi, tawi la Ushia katika Uislamu, na wanaoishi Kaskazini ya Yemen wanafungamana na Iran. Baina ya mwaka 2004 na 2010 walijaribu mara sita kuendesha uasi na majeshi yao yaliwasili hadi mji mkuu wa Sanaa. Wao wanahisi wanabaguliwa kwa kunyimwa nyadifa muhimu serikalini.
Kuna pia kundi la tatu ambalo ni muhimu katika hatima ya nchi hiyo, nalo ni Harakati ya Ukombozi wa Yemen Kusini ambalo linapigania sehemu ya Kusini ya Yemen iwe huru kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 1990 pale sehemu mbili za Yemen- ya Kaskazini na Kusini- zilipoungana tena.
Kutokana na yale yaliyoitwa Machipuko ya Kiarabu hapo mwaka 2011, kwa mara ya kwanza mambo yalianza kuchemka. Uliitishwa Mkutano wa Mdahalo wa Kimataifa kuandaa Katiba Mpya ya nchi. Mkutano huo ulitakiwa utunge mfumo wa Serikali ya Shirikisho pamoja na kuwapo usawa na haki baina ya mikoa.
Lakini mwishowe ulishindwa kufikia makubaliano. Septemba 2014 viongozi wa Wahouthi waliwaachilia wapiganaji wao waukamate Mji Mkuu wa Sanaa. Na pale Rais Hadi mwanzoni mwa 2015 ilipombidi akimbie kutoka mji huo, Mohammed bin Salman alitangaza vita vya kuivamia Yemen kwa kisingizio cha kutaka kuirejesha madarakani serikali halali ya Rais Hadi.
Mohammed bin Salman ndiye aliyetoa amri ya kuanzishwa vita vya Yemen ambavyo vimegharimu dola bilioni 60 kila mwaka. Hadi sasa hakuna upande ulioshinda kwa vile jeshi la Saudi Arabia ambalo lina silaha nzito nzito halijaweza kuwaangamiza wapiganaji wa Kihouthi.
Kwa mwezi wa nne sasa Wasaudi na washirika wao, wakiwa na wanajeshi 10,000, wameizingira na wanaishambulia bandari ya Hodeidah iliyoko katika Bahari ya Sham na inayoshikiliwa na Wahouthi. Asilimia 80 ya bidhaa zinazoenda Yemen, ikiwamo misaada ya kimataifa, zinapita katika bandari hiyo.
Matokeo ya mapigano juu ya bandari hiyo ndio yatakayoamua hatima ya vita vizima vya Yemen. Japokuwa Wasaudi kwa zaidi ya miaka miwili walitangaza kwamba ushindi kwao uko karibu kufikiwa, lakini jambo hilo hilijaonekana hadi sasa.
Wachunguzi wa mambo wanasema Wasaudi wamekwama katika matope ya Yemen kama vile Wamarekani walivyokuwa katika Vita vya Vietman mnamo miaka ya sitini na sabini.
Kila mtu anajua wazi kwamba pindi leo Marekani na Uingereza zikimwambia Mrithi wa Ufalme Mohammed bin Salman kwamba Vita vya Yemen lazima vikome, basi jambo hilo litafanyika. Sehemu kubwa ya silaha walizonazo Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zinatokea Marekani na Uingereza.
Bila ya madege ya Kimarekani yanayoweza kutia mafuta ndege nyingine hewani, ndege za kijeshi za Saudi Arabia hazitaweza kila wakati kuruka juu ya anga ya Yemen. Katika kituo cha kijeshi huko Riyadh mabingwa wa Kimarekani na Kiingereza ndio wanaosaidia kuchagua malengo yanayofaa kushambuliwa.
Mengi ya malengo yanayokusudiwa hukosewa kufikiwa na badala yake raia wengi wasiokuwa na hatia huuawa na miundombinu kuharibiwa.
Mambo yamezidi kuwa magumu hivi sasa. Mwanzoni mwa vita hivi Saudi Arabia na Qatar zilikuwa bega kwa bega katika kuwapiga vita Wahouthi. Lakini hali imebadilika tangu pale Riyadh kuituhumu Doha kwamba inawaunga mkono magaidi.
Mawaziri kadhaa wa serikali ya uhamishoni ya Rais Hadi wanasemekana wana maingiliano mazuri na Qatar na pia na Chama cha Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood) ambacho kinatajwa na Wasaudi kuwa ni cha kigaidi.
Licha ya hayo, Umoja wa Falme za Kiarabu ni kaidi zaidi katika kuviendeleza vita hivi kuliko hata Saudi Arabia. Majeshi ya Abu Dhabi yako usoni kabisa katika vita vya nchi kavu huko Yemen.
Vita hivi vimewachosha watu wengi duniani. Machi 2018, ikiwa imetimia miaka mitatu tangu vianze, maseneta wa Kimarekani wa Chama cha Democratic walichachama kwa mara ya kwanza kupinga namna vita hivyo vinavyoendeshwa.
Maseneta hao 44 walilaumu, huku wengine 55 wakiridhia. Hata hivyo, mambo huenda yakabadilika katika miezi michache ijayo kutokana na kuuliwa Jamal Khashoggi na pia kutokana na pigo ililopata utawala wa Rais Trump katika uchaguzi wa Bunge la Marekani hivi karibuni.
Waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry, mwaka 2016 aliweza kuzikutanisha pande zinazoshiriki katika vita hivi katika mazungumzo yaliyofanywa Kuwait. Yeye aliwasilisha muswada wa kusitisha mapigano.
Lakini alipoingia madarakani Donald Trump mzozo wa Yemen haujapewa umuhimu. Sasa yaonesha, baada ya kuuliwa Khashoggi, utawala wa Trump unaanza polepole kujitenga na siasa ya maangamizi ya Saudi Arabia katika Yemen.
Waziri wa ulinzi wa Marekani, Jim Mattis, sasa ametaka mapigano yasitishwe. Hayo ni mabadiliko makubwa katika siasa ya Marekani na jambo hilo linaungwa mkono na Waziri wa Mambo ya Kigeni, Mike Pompeo.
Serikali ya Washington inataka pande zinazopigana zikutane mwezi huu wa Novemba huko Sweden chini ya usimamizi wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa juu ya Yemen, Martin Griffith, ili kutafuta suluhisho la kisiasa. Mattis anachukulia kwamba Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zitakuwa tayari kushiriki.
Pompeo anataka mashambulio yote ya maroketi kutoka kwa Wahouthi kuelekea ardhi za Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu yasitishwe na pia mashambulio ya majeshi ya anga ya Nchi za Muungano kuelekea maeneo ya Yemen yanayokaliwa na raia.
Nayo Ujerumani, kupitia Waziri wake wa Mambo ya Kigeni, Haiko Maas, inaunga mko wazo hilo la Marekani na  kusema kwamba huu ndio wakati mwafaka wa kuitisha mkutano huo.
Utashi huu mkubwa wa ghafla uliochomoza kutaka vita vya maangamizi vya Yemen vimalizwe umetokana pia na mshtuko mkubwa iliyopata dunia kutokana na kifo cha Mwandishi Habari wa Kisaudi, Jamal Khashoggi, aliyeuliwa kikatili mwezi uliopita ndani ya jengo la ubalozi mdogo wa nchi yake mjini Istanbul, Uturuki.
Ikiwa wakuu wa Saudia wamediriki kumuua raia wao wenyewe ndani ya jengo la ubalozi wao, walimwengu, wakiwamo Wamarekani, wanahisi umewadia wakati sasa kwa Wasaudia pia wabinywe ili wayakomeshe maafa wanayoyasababisha huko Yemen.