Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), limeufungia wimbo wa kushirikiana wa wasanii, Raymond Mwakyusa (Rayvanny) na Naseeb Abdul (Diamond Platnumz) unaoitwa ‘Mwanza’ huku sababu moja wapo ya kufungiwa ikiwa ni kutaja jina la mcheza video maarufu, Amber Rutty anayekabiliwa na kesi ya kusambaza video akifanya mapenzi kinyume ma maumbile.
Akizungumza na Mtanzania Digital leo Jumatatu Novemba 12, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza amesema pamoja na kuufungia wimbo huo wametaka wasanii hao wauondoe mtandaoni kwasababu hauna maadili na haufai kusikilizwa na jamii.
Pia Mngereza amesema wamewaandikia barua ya kuwaita Diamond na Rayvany katika ofisi za Basata kwa mazungumzo zaidi.
“Pale WCB kuna hadi viongozi wa serikali lakini wanafanya kazi bila kufuata sheria na kanuni za Basata na wanazijua pia hawa ni wasanii waliosajiliwa na baraza hili wanajua hairuhusiwi msanii kutoa kazi bila kuletwa kwetu kwa ukaguzi.
“Na katika hilo tamasha lao la Wasafi Festival ni marufuku kutumia nyimbo zilizofungiwa kwa namna yoyote ile,” amesema Mngereza.
Aidha Mngereza ametoa rai kwa wasanii wote nchini wenye kazi zao za sanaa wapeleke Basata kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kuzitoa lakini pia wazingatie maadili ya Kitanzania.