27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wafanyabiashara wa madini walia na Serikali

    Na PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

WAFANYABIASHARA wanunuzi na wauzaji wa madini Tanzania (Tamida), wameiomba Serikali kutoa zuio kwenye uuzaji wa madini ghafi yenye thamani ya chini (cheapstone) ili waweze kufufua soko la madini hayo ambalo lilichangia kuongeza pato la taifa.

Kauli hiyo imekuja mwaka mmoja baada ya Serikali kuzuia uuzaji wa madini hayo tangu Julai mwaka jana.

Walidai kuwa suala la uzuiaji wa biashara ya makinikia nalo limechangia kukosekana kwa mapato ya Serikali.

Wakati wakitoa kauli hiyo, Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, juzi ilieleza changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2017/18 ni pamoja na kupunguzwa kazi kwa wafanyakazi wa migodi.

Dk. Mpango aliyasema hayo bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa na mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya mwaka 2019/20.

“Changamoto kubwa zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2017/18 ni pamoja na ugumu wa kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara waliopo kwenye sekta isiyo rasmi, kwa kuwa hawana sehemu rasmi na za kudumu za kufanyia biashara na hawatunzi kumbukumbu.

“…Vilevile kodi hizi zimeathirika kutokana na kupunguzwa kazi kwa wafanyakazi kwenye migodi ya madini kufuatia kupungua kwa shughuli za uchimbaji madini kwa baadhi ya migodi,” alisema Dk. Mpango.

Jana wafanyabiashara wa madini walikutana Dar es Salaam na kutoa tamko kupitia mwenyekiti wao wa Tamida, Sammy Mollel ambaye alisema tangu zuio hilo litolewe, wamekuwa wakiitumia nchi ya Kenya kuuza madini hayo.

Alisema Serikali inapaswa kuliangalia upya zuio hilo pamoja na kurekebisha sheria ambazo zinabana uwepo wa soko hilo hatua ambayo imechangia kukosa mapato.

“Cheapstone inapatikana katika nchi mbalimbali za Afrika, lakini waliifanya Tanzania kuwa kitovu cha soko kuu la madini hayo ambapo wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali duniani walikuwa wanakuja kuuza na kununua, lakini zuio hilo limesababisha wafanyabiashara hao kupeleka soko hilo nchini Kenya,” alisema Mollel.

Alisema hadi sasa baadhi ya masonara nchini wamefunga maduka kutokana na kukosa bidhaa hizo ambazo kwa sasa zimekuwa adimu.

“Awali kabla ya zuio hilo, wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi walikuwa wakiuza zaidi ya tani 400 kwa mwezi, ambapo kilo moja ya madini hayo uuzwa dola za Marekani 2,000. Hivyo basi Serikali inapaswa kuangalia upya zuio hilo kwa sababu mapato yanapotea,” alisema Mollel.

Alisema mkakati wao ni kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha wanapata mapato yatokanayo na madini ghafi, jambo ambalo linaweza kuisaidia kupata fedha ambazo zitatumika kwenye shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa.

Naye Mjumbe wa Tamida, Osman Tharia aliiomba Serikali kuangalia upya sheria zinazosababisha madini hayo kuzuiwa ili ziweze kufanyiwa marekebisho ambayo yataruhusu madini hayo kupatikana na kuuzwa nchini.

“Baadhi ya masonara wenzetu wamefunga maduka kutokana na ukosefu wa madini hayo kwa sababu hauwezi kutengeneza vito bila ya kutumia madini, hivyo basi tunaiomba Serikali kuangalia upya suala hilo,” alisema Tharia.

Alisema pia wameiomba Serikali kutoa elimu kwa masonara ili waweze kujua kiasi cha kodi wanachopaswa kulipa kuliko kukadiria kwa sababu kumechangia kujitokeza kwa malalamiko.

“Masonara wanalalamika kutozwa kodi kubwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa sababu hawana elimu ya kutosha ya ulipaji wa kodi, hivyo basi mamlaka husika inapaswa kuwaita na kuwapa elimu ili kuepusha malalamiko hayo,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles