*Adai Coastal Union imewaongezea kasi
*Aiandalia dozi Tanzania Prisons kesho
NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Yanga Mholanzi, Hans van Pluijm, ameanza kupiga hesabu za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanaoushikilia, akidai ushindi waliopata juzi dhidi ya Coastal Union utawaongezea kasi ya kutimiza hilo.
Mabingwa hao wameanza kwa kishindo kutimiza lengo lao hilo msimu huu kwa kuichapa Coastal Union mabao 2-0 kwenye mechi ya ufunguzi yaliyofungwa na Simon Msuva na Mzimbabwe, Donald Ngoma.
Ikumbukwe ya kuwa kwenye mechi yao ya mwisho waliyocheza msimu uliopita kwenye uwanja huo, Yanga iliipa kipigo kikali Coastal Union cha mabao 8-0.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini hapa, Pluijm alisema amefurahishwa na ushindi huo na anaamini utamuongezea kasi ya kufanya vizuri katika mechi zinazofuata ikiwemo ya kesho watakayoikaribisha Tanzania Prisons.
“Ushindi huu umezidi kutuongezea kasi. Tunahitaji kushinda na kuongoza kwenye michezo ijayo ili kutetea ubingwa.
“Nawapongeza vijana wangu kwa mchezo mzuri waliouonyesha ingawa tumekutana na timu ngumu ambayo nilijua itatupa wakati mgumu tangu mwanzo kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao kocha wao,” alisema.
Alisema wachezaji wake wameweza kutengeneza nafasi nyingi sana za kufunga mabao lakini wameshindwa kuzitumia na kudai jambo hilo halikuweza kuwaharibia mipango ya kuchukua pointi.
“Licha ya timu yangu kufanya vizuri lakini kulikuwa na makosa madogo madogo ambayo nitayarekebisha kabla ya kukutana na Tanzania Prisons…Nawapongeza Coastal Union kwa mchezo waliouonyesha na jinsi walivyotoa upinzani mkubwa kwa timu yangu,” alisema.
Ushindi huo umeifanya Yanga kukaa kileleni kwa pointi tatu ikiwa ni baada ya kufunga mabao mawili bila kuruhusu wavu wake kuguswa.
Mara ya mwisho Yanga kukutana na Prisons ilikuwa ni kwenye mchezo wa kirafiki mkoani Mbeya mwezi uliopita, Yanga ilishinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Amissi Tambwe na Malimi Busungu, vile vile msimu uliiopita kwenye ligi ikailaza mabao 3-0.