Na MWANDISHI WETU, KIBAHA
MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, amekataa kuzindua kituo kikubwa cha kisasa cha mabasi yanayokwenda mikoani kilichopo Maili Moja Kibaha mkoani Pwani.
Vilevile ametaka ufanyike uchunguzi wa kasoro zilizopo kabla ya kukizindua.
Alitoa uamuzi huo jana baada ya kufika katika kituo hicho ambako alieleza wasiwasi wake kuhusu utekelezaji wa mradi huo ikiwamo kubaini upungufu mbalimbali.
Makamu wa rais aliagiza ufanyike uchunguzi ndani ya wiki tatu na baada ya kukamilika atarudi kukizindua.
Alisema kuna minong’ono kuhusu mradi huo hivyo ni jukumu lake kuibeba na atakapojiridhisha atarudi kwa mara nyingine .
Samia aliahidi kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, mkurugenzi na Mkuu wa Mkoawa Pwani kuzungumzia suala hilo na kutafuta ufumbuzi wa pamoja.
“Msishtuke kwa hili ni kawaida kuchukua hatua za aina hii kujiridhisha kwa masilahi ya halmashauri, mkoa na watumiaji pia.
“Serikali ya CCM ni sikivu na tumesikia malalamiko ya wananchi. Tumepata malalamiko kidogo kuhusu stendi hii, serikali ni ya uwazi na ukweli hivyo sitofungua stendi,” alisema Samia.
Alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Jennifer Omolo na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama na wahusika waliohusika kufanikisha mradi huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema wapo wataalamu wanaohakiki lakini yeye kama ameridhishwa na kazi hiyo.
“Kwani kila kazi ina changamoto za ubinadamu, hasi na chanya, lakini wamejitahidi,” alisema Jafo.
Alisema mradi wa ujenzi wa kituo hicho umepata msaada wa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia wa dola za Marekani milioni 255, ambao unagusa kwenye miji 18 na kujenga vituo vipya tisa, barabara za miji kwa kiwango cha lami na madaraja makubwa.
Awali, madereva wa bodaboda, walidai licha ya ujenzi wa kituo hicho cha kisasa, bado hakuna sehemu ya kujikinga jambo ambalo litawaleta usumbufu wakati wa mvua na jua kali.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Omolo alisema mradi wa ujenzi wa kituo hicho umegharimu Sh bilioni 2.9 na mkandarasi amekwisha kulipwa bilioni 2.7.