27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kigogo mwingine Acacia kortini kwa utakatishaji fedha

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Acacia Tanzania, Asa Mwaipopo (55), ameunganishwa katika kesi inayowakabili vigogo wengine wa kampuni hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mwaipopo alisomewa mashtaka tisa yakiwamo ya kula njama, kughushi, kuongoza uhalifu wa kupangwa, ukwepaji kodi na utakatishaji fedha.

Katika hati ya mashtaka ya ukwepaji kodi yako matatu, kughushi lipo moja na kutakatisha fedha matatu.

Akisoma hati ya mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi akisaidiana na Jackline Nyantori, alidai   kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30, 2017 mshtakiwa   alitenda makosa hayo katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam, Kahama, Tarime, Biharamulo, Johannesburg Afrika ya Kusini, Toronto, Canada na Uingereza.

Ilidaiwa kuwa katika kipindi hicho na katika maeneo hayo, aliongoza uhalifu wa kupangwa kwa kutoa msaada katika usimamizi wa utendaji wa mpango wa uhalifu kwa lengo la kupata faida.

Katika shitaka la ukwepaji kodi, Wakili Nchimbi alidai   kati ya Mei 16,2008 na Desemba 11, 2008 mshitakiwa  alitoa tamko la uongo kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA  kwa nia ya kukwepa kodi Dola za Marekani 9,309,600.

Katika shitaka la kutakatisha fedha, Wakili Nyantori alidai   kati ya Mei 16 na Mei 25, 2008 mshitakiwa alishauri na kuisaidia Kampuni ya Madini ya Pangea kujipatia Dola za Marekani 9,309,600.

Aliendelea kudai kuwa katika shtaka jingine la kutakatisha fedha, mshitakiwa alijipatia Dola za Marekani 9,309,600 huku akijua fedha hizo ni zao la makosa ya kugushi na kukwepa kodi.

Mshtakiwa huyo anadaiwa pia kati ya Mei 16 na Desemba 31, 2008 alikwepa kodi Dola za Marekani 840,000 ambayo ni kodi ya zuio iliyotokana na mizunguko ya fedha kutoka Tulawaka iliyopaswa kulipwa TRA.

Mshitakiwa   anadaiwa kati ya Mei 16 na Mei 25, 2008 alishauri na kusaidiana na Kampuni ya Madini ya Pangea na Exploration Du Nord Ltee, kujipatia Dola za Marekani 840,000 wakijua ni zao la makosa tangulizi ya kugushi na kukwepa kodi.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, upande wa mashitaka ulidai   upelelezi   haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo upande wa utetezi uliiomba mahakama upelelezi wa shauri hilo uharakishwe   haki itendeke kwa sababu mambo hayo yalitokea miaka mingi iliyopita na makosa hayo hayana dhamana.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 31 mwaka huu itakapotajwa tena.

Wiki iliyopita vigogo wengine wa Acacia, Deogratias Mwanyika na mwenzake Alex Lugendo walipandishwa kizimbani hapo na kusomewa mashitaka 39.

Wanadaiwa kuwa kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30, 2017, kwa pamoja walitenda makosa hayo katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam, Kahama, Tarime, Biharamulo, Johannesburg Afrika ya Kusini, Toronto, Canada na Uingereza.

Wanadaiwa kula njama, kugushi, kutakatisha fedha, kukwepa kodi na kutoa rushwa ya Dola za Marekani milioni 7.1 kwa aliyekuwa Mkuu wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Shinyanga, Hussein Kashindye kumshawishi asiweze kufanya uchunguzi kwenye Kampuni ya Bulyanhulu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles