31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Necta yaanika mtandao wizi wa mitihani

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

BARAZA la Mitihani la Tanzania (Necta), limefichua mtandao wa wizi wa mitihani huku likifuta matokeo ya watahiniwa 357 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) 2018.

Necta pia imezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 120 ambao waliugua ama kupata matatizo na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au baadhi ya masomo.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alizishauri mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua wote waliosababisha udanganyifu kwenye mtihani huo uliofanyika Septemba 5 na 6, mwaka huu.

Oktoba 2, mwaka huu Necta ilitangaza kubaini wizi wa mitihani na kuamuru shule zote za Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma, Shule ya Kondoa Integrity (Kondoa, Dodoma), Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy (Dar es Salaam), Alliance, New Alliance na Kisiwani za Mwanza zirudie mtihani huo.

Mbali na hilo, Oktoba 9, mwaka huu Necta pia ilizitaja shule nyingine zilizoongezeka katika mtandao huo wa wizi kuwa ni Atlas (Ubungo), Atlas (Madale) na Great Vision zote za Dar es Salam ambazo pia wanafunzi walirudia mtihani huo.

 

MTANDAO WA WIZI

Jana akizungumzia mtandao wa wizi, Dk. Msonde alisema wamiliki wa shule zilizohusika walitumia kituo teule cha Shule ya Msingi Nyanduga iliyopo Halmashauri ya Rorya mkoani Mara kuiba mtihani.

Dk. Msonde alisema bahasha za mitihani zilizokuwa zikitunzwa katika kituo hicho zilikuwa zikichanwa na mitihani kusambazwa kwa njia ya WhatsApp hadi shule za Fountain of Joy na Aniny Ndumi.

Alisema shule hizo nazo zilisambaza kwenda shule za Alliance, New Alliance, Hazina, New Hazina, Atlas Ubungo, Atlas Madale na Great Vision.

“Uovu huo ulifanikishwa kwa kusaidiwa na viongozi wa elimu wa Halmashauri ya Rorya akiwemo Ofisa Elimu Msingi, Zacharia Weibina (aliyekuwa Kaimu Ofisa Elimu Taaluma Rorya).

“Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu, Thobias Ojijo (aliyekuwa Kaimu Ofisa Elimu Rorya), Ofisa Elimu Kata, Omary Killo (aliyekuwa mkuu wa msafara) na Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Nyanduga, Marwa Mtatiro,” alisema Dk. Msonde.

Alitaja wengine waliohusika kuwa ni aliyekuwa Msimamizi Mkuu Shule ya Msingi Nyanduga na askari G.6098 D/C Gicibert aliyekuwa analinda chumba madhubuti (strong room) katika kituo teule cha Nyanduga.

Dk. Msonde alisema katika hali ya kushangaza, aliyekuwa akisambaza mitihani alianza kuisafirisha saa saba usiku.

“Hii ilikuwa mkakati uliopangwa kwahiyo ilikuwa danganya toto, kwa sababu huwezi kusafirisha mtihani saa saba usiku kwenda sehemu husika ambayo ni kilomita 16 tu,” alisema.

 

UDANGANYIFU

Pamoja na hilo, Dk. Msonde alisema baadhi ya walimu wakuu na wasimamizi wasio waaminifu walishiriki katika vitendo vya udanganyifu wakati mitihani ilipokuwa ikiendelea.

Alisema katika Shule ya Msingi Liwale, Halmashauri ya Liwale mkoani Lindi, Mwalimu Mkuu Lucius Matendo alikula njama na wasimamizi wa mtihani na kukubaliana kutoa nje karatasi ya maswali mara bahasha yenye mitihani ikishafunguliwa.

Dk. Msonde alisema Mwalimu Matendo alikuwa anatafuta majibu na kuwapatia watahiniwa walioandaliwa.

“Ofisa ufuatiliaji wa baraza alipofika shuleni alibaini uwepo wa njama na kufanikiwa kumkamata mtahiniwa mmoja aliyekuwa na majibu yaliyotafutwa na mwalimu mkuu, mtahiniwa alikiri na kufafanua uwepo wa njama na kutaja wahusika wake.

“Uchunguzi zaidi ulipofanyika kwenye kazi za watahiniwa umethibitisha kuwepo kwa mfanano usio wa kawaida wa kazi za watahiniwa. Majibu yao yanafanana na majibu yaliyopo kwenye karatasi iliyoandikwa na mwalimu mkuu,” alisema Dk. Msonde.

Aina ya pili ya udanganyifu waliyobaini ni ile ya Shule ya Msingi Mwekako, Halmashauri ya Chato mkoani Geita, ambako wasahishaji walibaini karatasi zilizotumika kujibia maswali ni tofauti na zilizotolewa na Necta.

Dk. Msonde alisema majibu ya watahiniwa hao yalikuwa na mfanano wa kupata na kukosa usiokuwa wa kawaida.

Alisema watahiniwa walipohojiwa walikiri kuwa majibu walikuwa wakipewa na Mwalimu Mkuu, Habibu Rweshabura Nuru.

“Uchunguzi zaidi umebaini kuwa mwalimu mkuu huyo alikula njama na wasimamizi wa mtihani na kukubaliana kutoa nje karatasi ya maswali mara tu baada ya bahasha yenye mitihani kufunguliwa.

“Mwalimu alihakikisha majibu yanatafutwa na watahiniwa wanajaziwa, utaratibu huu ulisababisha kuwapo karatasi za kawaida tofauti na zilizoandaliwa,” alisema.

Dk. Msonde alisema katika Shule ya Msingi Bariadi Alliance mkoani Simiyu, walimu Simon Shepard, Ogwang Andrew na Thomas Malongo walifanya kikao maalumu cha kuweka mkakati wa kufanya udanganyifu wakati mitihani itakapokuwa ikifanyika.

Alisema walimu walipanga kula njama na wasimamizi kutoa karatasi ya maswali nje ya chumba cha mtihani baada ya kufungua mtihani huo.

Dk. Msonde alisema walimu hao walikokotoa majibu na kuyaandika kwenye rula tano ambazo walipewa watahiniwa watano ili wafikishe majibu hayo pia kwa baadhi ya wanafunzi waliokuwa wamepangwa kuoneshwa.

“Wakati wa utekelezaji, ofisa mfuatiliaji alizikamata rula hizo na katika mahojiano watahiniwa walikiri kosa na kufichua mpango mzima kama ulivyofafanuliwa,” alisema.

Vile vile alisema wakati mtihani wa somo la Sayansi ukiendelea kufanyika, msimamizi Faustine Mtesigwa aliwakamata watahiniwa wawili wakiwa na karatasi zenye majibu katika Shule ya Msingi Msufini mkoani Geita.

“Uchunguzi zaidi uliofanyika umebaini mfanano usiokuwa wa kawaida wa majibu ya kupata na kukosa kwenye somo la Kiingereza na Hisabati ya watahiniwa wa shule hiyo ya Msufini.

“Katika masomo mengine, uchunguzi ulibaini kuwa katika somo la Hisabati, baadhi ya watahiniwa walikosa swali la 41 kwa kuandika jibu +27 badala ya -27.

“Imebainika watahiniwa wote walikosea jibu kutokana na aliyewaonesha kukosea kunakili swali kwa kuweka -6 badala ya +6 iliyokuwa kwenye swali.

“Mfanano huo unaonesha kuwa uongozi wa shule ulishirikiana na baadhi ya wasimamizi kufanikisha udanganyifu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles