32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Simulizi chungu ya kutekwa Mo

Na ANDREW MSECHU – dar es salaam

MSAMARIA aliyemsaidia mfanyabiashara Mohamed Dewji (Mo) kupata simu na kumpigia baba yake mara baada ya kutelekezwa na watekaji wake eneo la Gymkhana, amesimulia namna alivyoonana na bilionea huyo kijana aliyekuwa amejisitiri kwa kitambaa huku akiwa kifua wazi.

Mtu huyo ambaye ni mlinzi katika Hoteli ya Southern Sun ya Dar es Salaam kupitia Kampuni ya Knight Support (jina linahifadhiwa), alieleza kuwa yeye ndiye aliyempokea na kumsitiri Mo, kisha kumpa mawasiliano yaliyomuunganisha na baba yake.

Akizungumza na MTANZANIA jana, msamaria huyo alisema Mo baada ya kutelekezwa na watekaji wake, alifika hotelini hapo akiongozana na mlinzi mmoja wa eneo jirani na alipotelekezwa.

Alisema alipomwona Mo, hakuweza kumtambua hadi pale alipojitambulisha kutokana na namna alivyoonekana kwani alikuwa amejifunga kipande cha kitambaa kinachoonekana kama vitambaa vinavyotumika kuweka matangazo barabarani.

“Kwa namna alivyokuwa amevaa, yeyote kwa haraka asingemtambua, kiunoni alikuwa amejifunga kitambaa kinachoonekana kama vile vya matangazo, akiwa amekivaa kama msuli, juu akiwa kifua wazi,” alisema.

Alisema Mo alifika hotelini hapo majira ya saa nane kasoro usiku, akiwa katika harakati ya kutafuta sehemu salama huku akiomba msaada wa kuwasiliana na ndugu zake.

Shuhuda huyo ambaye alikuwa katika eneo la hoteli ya Southern Sun usiku wa kuamkia Jumamosi ya Oktoba 20, alilieleza MTANZANIA kuwa hakutarajia kumwona mfanyabiashara huyo katika mazingira hayo, hasa kutokana na hali aliyokuwa nayo.

“Alifika hapa akiwa ameongozana na mlinzi mwenzetu ambaye alikuwa akifanya doria katika majengo ya mbele hapa ambayo yana balozi za Umoja wa Ulaya.

Inaonekana alipita mbele ya jengo la Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) akiwa kifua wazi, sikumtambua hadi alipojitambulisha. Nilihamaki, sikutarajia,” alisema.

Aliongeza kuwa Mo alipita mbele ya Kituo Kidogo cha Polisi cha Kivukoni ambacho hufanya kazi mchana tu na usiku huwa kinafungwa.

Msamaria huyo alisema huenda Mo alitarajia kupata msaada wa polisi kituoni hapo, lakini hakufanikiwa, hivyo kujikuta akiendelea kuangalia namna ya kupata msaada.

Alisema Mo baada ya kutelekezwa, alijaribu kusogea kutafuta msaada hadi alipomwona askari huyo na kumwita kwa sauti, kisha kujitambulisha kuwa yeye ni nani na kumwomba amsaidie kumfikisha kwenye Hoteli ya Holiday Inn.

“Kwa wakati huo, kutokana na hali aliyokuwa nayo, yule askari alimshauri kwamba Holiday Inn ni mbali, eneo la karibu anapoweza kupata sehemu ya kupumzika ni hapa, kwa sababu ni umbali ambao haufiki hata mita mia moja, kwa hiyo akamleta hapa.

“Kwa mtu wa kawaida angeweza kudhani kuwa ni miongoni mwa machizi wanaozurura hovyo mitaani, tena kwa usiku ule hakuna mtu ambaye angemtambua kirahisi. Alipofika tu hapa, baada ya kujitambulisha nilihamaki, sikutarajia kuwa anaweza kuwa yeye,” alisema.

Alisema suala la kwanza ambalo Mo aliomba ni kumhakikishia usalama wake kwa wakati huo, na kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa msimamizi wa lindo usiku huo, aliwaita askari wake wanne ambao walimzingira kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kumdhuru.

Baada ya kumhakikishia ulinzi, alisema kuwa walimpa shati kisha kuendelea na mazungumzo na hatua ya kwanza aliomba mwenye mawasiliano ampigie simu mke wake, ili amweleze kuwa yuko huru kutoka mikononi mwa watekaji.

“Alituomba tumpigie mkewe simu, lakini nilimshauri kwamba kwanini asimpigie mtu mwingine kwa kuwa kwa mkewe anaweza kumshtua sana, hasa ukizingatia roho za akina mama zilivyo, ndiyo akatupa namba ya baba yake na mimi ndiye niliyetumia simu yangu kumpigia baba yake kumweleza kuwa mwanaye yuko hapa na kisha alizungumza naye mwenyewe,” alisema.

Alisema baada ya Mo kumthibitishia baba yake kuwa taarifa hizo zinatoka kwake, alifika hotelini hapo baada nusu saa akiwa na ndugu yake Mo, wote wakionesha kutoamini kama taarifa hizo ni za kweli.

“Baba yake alifika hapa akiwa kama haamini amini, alipomwona Mo alifurahi sana, akamkumbatia, akaongea naye maneno machache huku akionesha kuhamaki,” alisema.

Alisema baada ya baba yake kumtambua, alizungumza nao na kuwaomba wamruhusu ampeleke nyumbani na kuwa atawapa polisi taarifa baada ya kufika nyumbani.

“Kwahiyo aliondoka hapa na baba yake, walitushukuru na Mo alisema anashukuru kwa msaada tuliompa, hakuwa na maneno mengi ila alisema atarudi kutushukuru,” alisema.

Alieleza kuwa karibu nusu saa baada ya Mo kuondoka na baba yake, majira ya saa tisa usiku ndipo gari ya polisi ilifika eneo hilo ikiwa na maofisa wa polisi ambao walidhani mfanyabiashara huyo yupo hotelini hapo.

“Tuliwaeleza kuwa Mo alifika hapa kuomba msada na tayari ameshachukuliwa na baba yake,” alisema.

Alisema polisi hao baada ya kufanya mahojiano ya kina walikubali kwa shingo upande hasa wakitaka waelezwe kwanini hawakupewa taarifa kwanza, lakini mwisho walikubali maelezo yao na kuondoka kwenda nyumbani kwa Mo.

“Kwa hali halisi ilivyokuwa, Mo wala hakuingia huko hotelini, aliishia hapa hapa nje na baba yake alikuja kumchukua hapa, wala hata uongozi wa hoteli haukujua kinachoendelea,” alieleza.

Alisema suala hilo walilibeba wao kama walinzi wa hotelini hapo na kulimaliza wao, kwa kuwa walihitaji kufanya stara kutokana na mazingira yaliyokuwepo.

MTANZANIA liliutafuta uongozi wa hoteli hiyo ambao haukuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba hawana taarifa yoyote kuhusu uwepo wa Mo hotelini hapo kwa muda na siku zinazotajwa.

Mo alitekwa nyara na watu wasiokjulikana alipowasili katika kituo cha mazoezi cha Hoteli ya Colloseum alfajiri ya Oktoba 11 na aliachiwa na watekaji hao usiku wa kuamkia Oktoba 20, siku tisa tangu alipotekwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles