Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Waziri wa wizara mbalimbali, Sophia Simba, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Ustawi wa Jamii.
Simba ambaye alifukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa usaliti, kabla ya kusamehewa na kurushwa kundini mapema mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais John Magufuli amewateua wenyeviti wengine wanne wa Bodi za taasisi za serikali baada ya waliokuwa wakiongoza bodi hizo kumaliza muda wao na wengine kuteuliwa katika nyadhifa nyingine.
Katika uteuzi huo, Profesa Anael Mkonyi, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mifupa (Moi), Mwamini Juma kuwa Mwenyekiti Bodi ya Sukari na Dk. Mwanza Kamata kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ambaye anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhandisi Christopher Chiza ambaye amechaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Buyungu.
“Rais Magufuli pia amemteua Dk. Maria Mashingo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo (TIB) akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Palamagamba Kabudi ambaye aliteuliwa kuwa Waziri na baadaye kuwa Waziri wa Katiba na Sheria,” imesema taarifa hiyo.